Sunday, 19 March 2017

SPANEST YAJA NA MPANGO WA FEDHA NA BIASHARA UTAKAOKUZA UTALIIMRADI wa Kuboresha Mtandao wa Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania (SPANEST) umekuja na Mpango wa Biashara na Fedha utakaosaidia maeneo hayo kusimamiwa vizuri ili yaongeze tija kwa Taifa na watu wake; tofauti na ilivyo sasa.


Mpango huo ulioandaliwa kwa miezi sita ulijadiliwa na kufanyiwa maboresho hivikaribuni jijini Mbeya katika kikao kilichoshirikisha wadau wa utalii na uhifadhi kutoka sekta mbalimbali za umma na binafsi.
 

Taarifa iliyotolewa katika kikao hicho ilieleza kwamba pamoja na maeneo hayo kuwa na rasilimali nzuri na zakipekee zinazoweza kuvutia kwa kiwango kikubwa watalii wa ndani na nje, yamekuwa yakiingiza kiasi kidogo cha fedha kwasababu yana changamoto mbalimbali.

Mratibu wa SPANEST inayoratibu mpango huo, Godwell Ole Meing’ataki alisema pamoja na kwamba mradi wa SPANEST unalenga zaidi katika kuyaboresha maeneo hayo, wanataka kuona yanapata fedha za kutosha kutokana na faida ya utalii ili yajiendeshe yenyewe.“Kabla ya kufika katika maeneo hayo na kulipa fedha, watalii wanatumia usafiri wa anga na ardhini, na wanapata huduma mbalimbali mahotelini na katika miji wanayopita, zote hizo ni fursa za biashara kwa watu na maeneo hayo; zikiboreshwa zitaleta faida kubwa,” alisema.

Alisema kwa kuwa na mpango wa fedha na biashara kutasaidia kuwa na dira ya mambo yanayotakiwa kufanyika ikiwa ni pamoja na namna ya kutoa huduma kwa watalii ili idadi yao iongezeke siku hadi siku na kuboresha miundombinu ya kufika katika maeneo hayo.

Meing’ataki alisema; “Ni muhimu tukatambua kwamba tunapofanya uhifadhi, tunakuza uchumi. Inawezekana  tusipate faida kubwa kupitia utalii lakini tunatakiwa kujua kuna faida zingine za kiuchumi zinazotokana na uhifadhi.”

Alitaja baadhi ya faida hizo kuwa ni pamoja na zile zinazotokana na utunzaji wa vyanzo vya maji kuwezesha shughuli za kilimo na uzalishaji wa nishati ya umeme na misitu kwa ajili ya kupunguza hewa ukaa.

Alisema kufanikiwa kwa mpango huo utakaokabidhiwa serikali baada ya kukamilika hivikaribuni kwa ajili ya kuanza kutumiwa, unahitaji ushirikiano wa serikali na taasisi zake, sekta binafsi na wadau wengine wa maendeleo.

Mtaalamu Elekezi anayefanya kazi ya kuuandaa mpango huo, Almasi Kashindye alisema dhana ya uhifadhi kwa kizazi kilichopo na kijacho ni muhimu ikafanywa kibiashara ili iongeze faida ambayo pia itawezesha usimamizi mzuri wa rasilimali za maeneo hayo.Alisema mapungufu ya kibiashara yaliyopo katika maeneo hayo yanatoa fursa kubwa zinazoweza kunufaisha na kuendeleza maeneo hayo na jamii, kifedha.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Chabo Africa ya mjini Iringa inayotoa huduma ya usafiri na kuongoza watalii, Ernest Lugalla alisema kuja kwa mpango huo kutasaidia kuboresha huduma hasa za hoteli zinazolalamikiwa na wageni wengi na hivyo kuzorotesha sekta hiyo.


“Baadhi ya hoteli zimekuwa zikitoza gharama kubwa kwa wageni pamoja na kukosa hadhi stahiki lakini pia  zinashida ya mawasiliano ya moja kwa moja," alisema.

Lugalla alizungumzia pia changamoto ya miundombinu ya barabara kwenda kwenye maeneo hayo huku akiita serikali kwa kushirikiana na mamlaka zinazohusika kuziboresha ili zipunguze gharama na muda kwa watalii wanaotembelea.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment