Sunday, 26 March 2017

RC MASENZA AWAITA WAWEKEZAJI WA HOTELI ZA NYOTA MKOANI IRINGA
MKUU wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza amewakaribisha wawekezaji wenye uwezo wa kujenga hoteli zenye hadhi ya nyota mkoani humo akisema mahitaji yake ni makubwa katika kukuza sekta ya utalii kusini mwa Tanzania.

Akifunga mafunzo ya siku tatu ya ukarimu na utalii yaliyofanyika mjini Iringa kwa uratibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Mradi wa Kuboresha Mtandao wa Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania (SPANEST), Masenza alisema mkoa una maeneo ya kutosha kwa ajili ya uwekezaji huo.

“Kwa upande wa manispaa ya Iringa, tayari tumeomba serikali ituachie eneo la Kihesa Kilolo na tayari imekubali, tutalipanga vizuri ili liwe la mfano kwa ajili ya kuhudumia utalii katika kanda ya kusini,” alisema.

Pamoja na wingi wa vivutio vya utalii katika kanda hiyo, Masenza alisema idadi ya watalii wa nje na wa ndani wanaovitembelea ni ndogo na moja ya sababu zake ni uchache wa huduma za kuhudumia watalii.

Akitoa takwimu za mwaka 2015, Mkuu wa Mkoa alisema ni asilimia nne tu ya watalii 764,837 toka nje ya nchi na asilimia nane tu ya watalii 641, 114 wa ndani waliotembelea vivutio vya mikoa ya kusini huku idadi kubwa iliyobaki wakitembelea vya kaskazini.

Alisema takwimu hizo zimewaongezea hamu ya kujipanga zaidi ili vivutio vya kanda ya kusini vipokee wageni wengi kama ilivyo katika mikoa ya kaskazini.

“Kwahiyo ni lazima kuwe na juhudi za pomoja kati ya serikali na wadau wa sekta binafsi ili azma hiyo ya kuchochea shughuli za utalii kusini ifanikiwe,” alisema.

Kwa upande wa sekta binafsi, Masenza alisema inatakiwa kuboresha huduma zake zikiwemo za ukarimu na utalii ili kuwashawishi watalii kutembelea zaidi kusini na kuwa mabolozi wazuri kwa wageni wengine.

Alisema kwa upande wake serikali itaendelea kutoa mafunzo ya muda mfupi, itasimamia kanuni zitakazoinua viwango vya huduma, itaboresha miundombinu ya barabara na viwanja vya ndege, itahimarisha uhifadhi wa maliasili na malikale na kutatua migogoro yake na itahakiki huduma za malazi na migahawa na kuziweka katika kiwango cha nyota.

Awali Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Utalii nchini, Paskas Mwiru alisema serikali imeamua kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa watoa huduma baada ya kubaini baadhi ya vyuo vinavyotoa mafunzo ya ukarimu na utalii nchini, vinayatoa chini ya kiwango.

Kwa kupitia mafunzo hayo, alisema watoa huduma wanapewa mafunzo katika maeneo ya mapokezi, utoaji wa huduma ya chakula na vinywaji, upishi na namna ya kukuza huduma ya malazi ili kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa katika sekta ya ukarimu na utalii katika mikoa ya kusini ambayo ipo chini.

Kwa kupitia mafunzo hayo, jumla ya wahitimu 80 kati ya zaidi ya 100 waliojitokeza wamefanikiwa kuhitimu na kutunukiwa vyeti walivyokabidhiwa na mkuu wa mkoa wa Iringa.Reactions:

0 comments:

Post a Comment