Wednesday, 22 March 2017

NAPE APOKEA RIPOTI YA KAMATI, MAKONDA AKACHA KUHOJIWA


Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye amepokea taarifa ya kina kuhusu chanzo, sababu na namna tukio la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda alipovamia kituo cha Utangazaji cha Clouds Media akiwa na walinzi wenye silaha za moto Machi 17, 2017.

Haya ndiyo maelezo ya Kamati hiyo yaliyotolewa na mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo Deudatus Balile.

Tulifanya mahojiano na wafanyakazi 14 wa kituo cha Clouds.­

Tulifanya jitihada za kumtafuta Mkuu wa Mkoa, tulimpigia simu lakini hakupokea.­ Balile “Hata tulipofika katika ofisi yake, aliondoka kupitia mlango wa nyuma.

 “Baada ya kushindwa kuonana naye, tukajiridhisha kuwa amechagua mwenyewe kutotumia fursa ya kuhojiwa”.

“Katika uchunguzi wetu, tumejiridhisha kuwa Mkuu wa Mkoa alivamia kituo cha Clouds akiwa anaendesha gari mwenyewe”. ­

“Kamati imejiridhisha kuwa RC na askari wenye silaha waliingia hadi ndani ya studio iliyokuwa ikirusha matangazo”. ­

‘Imebainika ni kweli alikwenda pale Clouds na askari, waliingia kwenye vyumba ambavyo walipaswa kuingia kwa idhini maalumu’­

“Kamati imejiridhisha pia kuwa palikuwa na vitisho kwa walinzi na wafanyakazi kwa kutumia askari wenye silaha”. ­

 “Miongoni mwa vitisho ni kuwalazimisha kurusha kipindi vinginevyo angewaingiza kwenye tuhuma za dawa za kulevya”.

 ‘Makonda aliwatishia wafanyakazi Clouds kuwa angewafunga miezi 6 pia angewaingiza kwenye orodha ya watuhumiwa wa dawa za kulevya’­

 “Baada ya hapo aliwatisha kuwa yote yaliyotokea usiku ule, yabaki pale pale ndani”

“Tumejiridhisha kuwa Mkuu wa Mkoa aliingilia taratibu za uhariri kwa kulazimisha habari anayoitaka iruke”

 “Kamati haikuona uthibitisho wowote kuwa kuna wafanyakazi waliopigwa na vitako vya bunduki au kupigwa mitama lakini walilia kwa vitisho vya kufungwa jela miezi sita bila kupitia mahakamani”

Tume Imebaini nini?
“Kamati imebaini kuwa vitendo vya mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Paul Makonda vina viashiria vya uvunjifu wa sheria mbalimbali za nchi hususani zinazohusiana na huduma za utangazaji na huduma za vyombo vya habari”­

“Kamati imeibaini kuwa mkuu wa mkoa anatumia vibaya madaraka yake”

“Clouds Media Group inastahili pongezi kwa kusimamia maadili ya uandishi wa habari”­

Mapendekezo ya kamati

Makonda awaombe radhi wafanyakazi wa Clouds Media na vyombo vyote vya habari

Waziri Nape Nnauye awasilishe rasmi malalamiko ya tasnia ya habari dhidi ya Makonda kwa mamlaka ya uteuzi wa mkuu wa mkoa kuomba achukuliwe hatua zinazopaswa

Vyombo vya dola vianzishe uchunguzi wa ndani dhidi ya askari waliongia na bunduki katika kituo cha utangazaji cha Clouds media

Kampuni ya Clouds Media ipitie upya miongozo ya kanuni,sheria na taratibu zinazoongoza shughuli za utangazaji ili kuwa na udhibiti wa watu wasiohusika kuzoea kuingia mara kwa mara na kufanya kazi za uhariri bila kuwa na taaluma ya habari.

Kauli ya Nape baada ya kupokea Ripoti

 “Nimeipokea ripoti ila siwezi kusema lolote kwa sasa, maana na mimi nina mamlaka za juu yangu. Kuna Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Rais. Nitawapelekea ripoti hii na ninaamini watachukua hatua. Nimeona watu wengi wakizungumza hisia zao kuwa ripoti itapuuzwa au ukweli utafichwa..Naomba wawe na subira”­

 “…Tumuamini Rais wetu mpendwa. Anaipenda tasnia ya habari. Yeye na mamlaka zingine zilizo juu yangu naamini watachukua hatua”

“Ripoti ina vielelezo vya sauti na picha za waliokuwa wanatoa ushahidi”­


 “Sisi tuliopewa dhamana ni vizuri kujifunza kuwa wanyenyekevu, kama binadamu tunaweza kukosea lakini tunaweza kurekebisha”

Reactions:

0 comments:

Post a Comment