Friday, 17 March 2017

MIJI YA KITALII YAWEZEKANA NYANDA ZA JUU KUSINI


MIKOA ya Nyanda za Juu Kusini itakuwa na miji ya kitalii kama ilivyo kwa miji kadhaa ya mikoa ya kaskazini ikiwa sekta ya hoteli na ubora wa huduma zake itakua kwa kasi inayotakiwa.

Mratibu wa Mradi wa Kuimarisha Maeneo ya Hifadhi Kusini mwa Tanzania (SPANEST), Godwell Ole Meing’ataki alisema pamoja na hoteli na huduma bora, wageni wanahitaji kutembea katika barabara nzuri ili kufikia vivutio hivyo.

Alitaja baadhi ya vivutio hivyo kuwa ni pamoja na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ambayo ni kubwa kuliko hifadhi zote nchini, hifadhi ya Taifa ya Kitulo, mapori ya akiba, hifadhi za jamii na misitu ya asili, safu za milima, fukwe za ziwa nyasa na maporomoko mbalimbali ya maji.

Akizungumza kwenye kikao cha wadau wa maliasili na utalii wa mkoa wa Njombe hivikaribuni, Meing’ataki alisema; “Kukua kwa sekta ya utalii na uhifadhi kutategemea sana ushirikiano kati ya sekta binafsi na ya umma pamoja na mchango wa wadau wengine.”

Alisema watoa huduma za hoteli ni wadau muhimu katika kukuza sekta ya utalii katika mikoa hiyo hivyo ni lazima watambue wajibu wao katika kutoa huduma bora zitakazowafurahisha na kuwavutia wageni wengi zaidi.

“Wakati wakitoa huduma hizo ni muhimu pia wakajua fursa au vivutio vya utalii vilivyoko katika mikoa yao,”alisema.

Akizungumzia maendeleo ya sekta ya hoteli katika mikoa ya kanda hiyo, Afisa Utalii wa Ofisi ya Kanda ya Utalii ya Nyanda za Juu Kusini, Sixtus Malangalila alisema mikoa ya Iringa, Mbeya, Njombe na Ruvuma inayounda kanda hiyo ina jumla ya hoteli 145 na kampuni za utalii 10 tu.

“Hoteli hizo ambazo hata hivyo hazikidhi vigezo vinavyotakiwa ili ziwe na sifa za hoteli pia hazikidhi mahitaji na huduma zinazotakiwa na wageni mbalimbali, wakiwemo wa nje ya nchi,” alisema.

Alisema wakati mkoa wa Iringa ambao ni kitovu cha utalii kusini mwa Tanzania una hoteli 28 tu, mkoa wa Mbeya una hoteli 63, Ruvuma 44 huku Njombe ukiwa na hoteli 10 ambayo ni idadi ndogo zaidi kwa mikoa hiyo.

Kwa upande wa kampuni zinazotoa huduma ya usafiri na kuongoza watalii, alisema mkoa wa Iringa una kampuni saba, Mbeya tatu na mikoa ya Njombe na Ruvuma haina kampuni hata moja.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment