Wednesday, 29 March 2017

KAMATI YA BUNGE YAMUHOJI MAKONDA


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Paul Makonda leo amehojiwa na Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuhusiana na tuhuma za kuingilia haki, uhuru na madaraka ya Bunge.

Mhe. Makonda aliwasili Bungeni  Dodoma majira ya saa nne asubuhi kuitikia wito wa Kamati hiyo uliotokana na Azimio la Bunge  lililotolewa na Bunge, Februari 8, 2017  katika Kikao cha Nane cha Mkutano wa Sita wa Bunge ambapo amehojiwa na kamati hiyo kwa muda wa masaa matatu kuhusu tuhuma zinazomkabili.

Katika kikao hicho, Bunge liliazimia kwamba Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Makonda na Mkuu wa Mkoa wa Arumeru, Mhe. Alexander Mnyeti kuitwa mbele ya Kamati ya Bunge ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge baada ya Bunge ili kujibu tuhuma hizo.

Akizungumza mara baada ya Kamati hiyo kumaliza kazi yake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Mhe. George Mkuchika alisema Kamati hiyo imekutana leo baada ya kuagizwa na Mheshimiwa Spika wa Bunge kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge.

“Tumefanya kikao hiki cha Kamati baada ya kuagizwa na Mhe. Spika kwa kuwa kwa Mujibu wa Kanuni zetu, Kamati hii inakutana pale tu inapoagizwa na Spika wa Bunge,” alisema.

Alisema Mhe. Spika aliiagiza Kamati hiyo imuite Mhe. Makonda mbele ya Kamati  kufuatia azimio hilo la Bunge lililopitishwa  na Bunge Februari 8, ambapo pamoja na mambo mengine Mkuu huyo wa Mkoa alitakiwa kufika mbele ya Kamati kujibu tuhuma hizo zinazomkabili.

Alisema kwa mujibu wa Azimio hilo, Mhe. Makonda alidaiwa kutoa kauli kupitia Televisheni ya Clouds akidai kwamba wabunge wanasinzia Bungeni jambo lililoonekana kwamba ni kudharau Bunge.

“Napenda kutoa taarifa kwamba Mhe. Makonda leo amekuja mbele ya Kamati na ametupa ushirikiano mzuri, tumepokea maelezo yake na Kamati imemaliza kazi yake,” alisema.

Alisema kama ilivyo utaratibu, Kamati yake itakabidhi taarifa yake kwa Mhe. Spika kwa mujibu wa Kanuni ambapo Spika ndiye atakaeamua namna ya kutoa raarifa kuhusu kazi ya Kamati hiyo


Reactions:

0 comments:

Post a Comment