Monday, 20 March 2017

JPM AMUOKOA MAKONDA DHIDI YA TUHUMA ZAKE

Tokeo la picha la magufuli, makonda

Rais, Dkt. John Pombe Magufuli amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuendelea kuchapa kazi bila kujali maneno ya mitandaoni.

Amesema kuwa yeye ni Rais anayeajiamini na hawezi kupangiwa na mtu kitu cha kufanya au nani awe wapi na awe nani.

Amesema kuwa anajua mambo mengi yanasemwa katika mitandao ya kijamii juu ya Makonda na kudai kuwa hata yeye anasemwa katika mitandao hiyo lakini anataka Mkuu huyo wa Mkoa aendelee kuchapa kazi kwani hakuna wa kumpangia kitu cha kufanya.

“Mnahangaika na vipost vyenu, wengine wanaingilia uhuru wangu, mimi sioneshwi njia ya kupita, mimi siingiliwi, ndiyo maana hata kuchukua fomu ya urais, nilikuwa peke yangu,” amesema Rais Magufuli na kuhoji kuwa hata mimi ninasemwa katika mitandao ya kijamii, je nijiuzulu Urais?

 Rais Magufuli amefunguka hayo leo wakati wa uzinduzi wa barabara za juu ‘Fly Over’ pamoja na Rais wa Benki ya Dunia, Dkt. Jim Yong Kim na kuwataka wakandarasi wa mradi huo wafanye kazi usiku na mchana huku akitoa onyo kali kwa wale watakaodiriki kufanya ubadhirifu wa mradi huo.

Hii ni mara ya kwanza kwa Rais huyo wa Benki ya Dunia kutembelea Tanzania. Benki ya Dunia hivi sasa inafadhili jumla ya miradi 23 ya kitaifa nchini yenye thamani ya dola za Marekani bilioni 3.6, na sehemu kubwa ya miradi hiyo inahusika na ujenzi wa miundombinu ya usafiri na miradi ya maendeleo vijijini.

Hivi karibuni Makonda amegonga vichwa vya habari katika mitandao ya kijamii na magazeti kuhusiana na kashfa ya kughushi vyeti vya kidato cha nne na kupelekea kuingia katika majibizano ya maneno na Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kuhusiana na sakata hilo la vyeti.

Makonda ambaye hivi karibuni alianzisha vita ya kupambana na madawa ya kulevya anadaiwa pia kuvamia studio za Clouds siku ya Ijumaa usiku akishinikiza kituo hicho kirushe video ya mwanamke aliyekuwa akidai kuzaa na Askofu Gwajima na kisha kutelekezwa na kiongozi huyo wa dini.


Tukio hilo limeibua hisia tofauti miongoni mwa wanajamii huku Waziri wa Habari, Nape Nnauye akifananisha tukio hilo kuwa sawa na kuinajisi tasnia ya habari na kuahidi kuunda kamati ya masaa 24 kuchunguza tukio hilo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment