Sunday, 19 March 2017

CHADEMA SH 500,000 CCM SH 100,000 UBUNGE AFRIKA MASHARIKI

Tokeo la picha la bunge la afrika mashariki

Baada ya Ofisi ya Bunge kutangaza kuwa Aprili 4 ni siku ya uchaguzi wa wajumbe tisa wa Bunge la Afrika Mashariki (Eala) kutoka Tanzania, vyama vya siasa vimeanza mchakato wa uteuzi.

Tayari vyama vya Chadema na CCM vimeshatoa masharti ya kuwania nafasi hiyo ikiwamo ada itakayotozwa.

Ofisi ya Bunge juzi ilitoa taarifa kuwa wenye nia ya kuwania nafasi hiyo watangaze kupitia kwenye vyama vyao vya siasa. Wajumbe wapya watachukua nafasi zinazoachwa wazi na Makongoro Nyerere, Shy­Rrose Bhanji, Bernard Murunya, Adam Kimbisa, Abdulla Mwinyi, Mariam Yahya Ussi, Angela Kizigha, Twaha Taslima na Nderakindo Kessy.

Bunge kupitia taarifa yake hiyo ilisema uteuzi utafanyika Machi 30 na uchaguzi utafanyika baada ya kipindi cha maswali na majibu bungeni.

Taarifa iliyotolewa jana na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Chadema, Tumaini Makene ilieleza mchakato ndani ya chama hicho umefunguliwa na uteuzi utafanyika Machi 22.

“Wanachama wote wenye sifa na vigezo vya kuwania nafasi hiyo kupitia Chadema wanatakiwa kuchukua na kujaza fomu za kuomba uteuzi huo,” alisema Makene.

Alisema vituo ambako fomu hizo zitapatikana ni ofisi za makao makuu ya chama hicho Mtaa wa Ufipa, Kinondoni jijini Dar es Salaam na ofisi zote za kanda 10 za Chadema Tanzania Bara na Zanzibar na ofisi za mikoa na majimbo.

Makene katika taarifa hiyo alisema mwanachama atakayechukua fomu anatakiwa kuambatanisha stakabadhi ya malipo ya ada ya Sh500,000 na wasifu wake, nakala ya cheti cha kuzaliwa au hati ya kusafiria.

Pia, anatakiwa kuwa na nakala ya kadi ya uanachama na kuwa na sifa za kugombea kama zilivyoainishwa kwenye ibara ya 67 ya Katiba ya nchi ya mwaka 1977.

Wakati huohuo, CCM katika taarifa yake iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole jana ilisema imepokea mwaliko kutoka kwa Katibu wa Bunge na fomu zitaanza kutolewa leo na mwisho wa kuzirejesha ni Machi 23 saa 10:00 jioni.

 Wakati ada ya fomu kwa Chadema ikiwa Sh500,000, CCM imesema zitatolewa kwa wanachama wake kwa ada ya Sh100,000.

Polepole alisema fomu zitatolewa makao makuu ya CCM Dodoma, ofisi ndogo za makao makuu Zanzibar na Lumumba, Dar es Salaam.Reactions:

0 comments:

Post a Comment