Sunday, 26 February 2017

SPANEST YAIWEZESHA NJOMBE KUANZISHA KAMATI SHIRIKISHI YA UHIFADHI WA MALIASILIMRADI wa Kuboresha Mtandao wa Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania (SPANEST) umeuwezesha mkoa wa Njombe kuwa wa kwanza kusini mwa Tanzania, kuunda mfumo shirikishi wa uhifadhi wa maeneo yaliyohifadhiwa ili kushughulikia kirahisi changamoto zake.

Kwa kupitia msaada huo, mkoa huo umeunda kamati itakayokuwa ikikutana kila baada ya miezi sita kujadili kwa pamoja namna ya kushughulikia changamoto za uhifadhi kwa kuzingatia sheria mbalimbali bila kuathiri upande mwingine.

Kamati hiyo inayoshirikisha Hifadhi ya Taifa Tanzania (TANAPA), mapori ya akiba, mamlaka za maji, hifadhi za jamii na misitu ya asili, halmashauri za wilaya, asasi za kiraia na watu binafsi iliundwa mwishoni mwa wiki katika kikao cha wadau wa Maliasili na Utalii wa mkoa huo.

Kama inavyotakiwa kufanyika katika mikoa mingine nchini, Mratibu wa SPANEST, Godwell Ole Meing’ataki alisema mkoa wa Njombe unatakiwa kutekeleza mfumo wa matumizi bora ya maliasili zake ili ziendelee kuwepo kwa manufaa ya sasa na  kizazi kijacho.

“Hiyo ni kutokana na changamoto zinatokana na matumizi yasio endelevu ya rasilimali hizo yanayosababishwa na ujangili, uhalifu wa kuua wanyama na mimea, ukataji na uchomaji miti misitu ya asili, kilimo kwenye mabonde na vyanzo vya maji na ufugaji katika maeneo yaiso ruhusiwa,” alisema.

Meing’ataki alisema kwa kupitia kamati hiyo na kwa kuzingatia sheria mbalimbali za uhifadhi wanyamapori, misitu na maji, changamoto mbalimbali zitakuwa zikijadiliwa na kutafutiwa mikakati ya kuzishughulikia kwa pamoja.

“Rasilimali zetu zitasalimika kama kila mmoja na kwa mfumo huu shirikishi atatimiza wajibu wake bila kuleta athari kwa mwingine,” alisema.

Awali Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Njombe, Lameck Noah aliwaambia wadau wa maliasili na utalii wa mkoa huo kwamba; “mkoa huu una rasilimali nyingi na kama zikitumika ipasavyo zitasaidia kukuza shughuli za utalii na pato la mkoa na mwananchi mmoja mmoja.”

Noah alivitaja baadhi ya vivutio vya utalii ambavyo ni rasilimali muhimu mkoani humo kuwa ni pamoja na hifadhi ya Taifa ya Kitulo, Pori la Akiba la Mpanga/Kipengere, misitu ya hifadhi, safu za milima Livingstone, fukwe za ziwa nyasa na mapromoko mbalimbali ya maji.

“Pamoja na kuvitambua vivutio hivyo kuna changamoto za usimamizi wake zinazohatarisha uendelevu wake,” alisema na kupongeza hatua iliyofikiwa na mkoa huo ya kuunda kamati shirikishi ya kusimamia maliasili.


Alisema mkoa utashirikiana na mamlaka zingine kuhakikisha maliasili zake zilizohifadhiwa zinalindwa dhidi ya vitendo vyovyote vya ujangili, hatua itakayosaidia pia kukuza shughuli za utalii ambazo zipo chini ikilinganishwa na mikoa mingine.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment