Tuesday, 28 February 2017

MPANGO WA KUPANDIKIZA WANYAMA HIFADHI YA TAIFA KITULO, WAIVA


SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) lipo katika hatua za mwisho zitakazowezesha Hifadhi ya Taifa ya Kitulo kupandikizwa aina mbalimbali za wanyamapori ili kuiongezea mvuto na kukuza shughuli za utalii nchini.

Kitulo ni hifadhi yenye zaidi ya spishi 350 za mimea jamii ya frola zikiwemo aina 45 za maua ya porini ambayo yamewafanya wenyeji waiite bustani ya Mungu huku wataalamu wa mimea wakiita Serengeti ya maua.

Pamoja na maua, hifadhi hiyo iliyopo wilayani Makete, mkoani Njombe ina aina mbalimbali za ndege wanaohama kati ya hifadhi hiyo na Ulaya na wanyama wengine jamii ya nyani wakiwemo Kipunji na kima.

Mhifadhi wa hifadhi hiyo, Fredrick Chuwa aliwataja wanyama wanaotarajiwa kupandikizwa hifadhini humo kuwa ni pamoja na Pofu, Pundamilia, Swala na wanyama jamii ya nyati.

Chuwa alisema tafiti mbalimbali zinaonesha wanyama hao waliokuwepo katika hifadhi hiyo miaka mingi iliyopita na wakapotea kwasababu mbalimbali ikiwemo ya ujangili.

“Mchakato wa kupandikiza wanyama hao unafanywa kwa ufadhili wa Shirika la Uhifadhi Wanyamapori na Mazingira-WCS, na mambo yakienda vizuri shughuli ya upandikizaji inaweza kuanza wakati wowote mwakani” alisema.

Alisema mpango huo umekuja huku Mradi wa Kuimarisha Maeneo ya Hifadhi Kusini mwa Tanzania (SPANEST) ukiendelea kuboresha hifadhi hiyo.

Mratibu wa SPANEST, Godwell Ole Meing’ataki alisema mradi huo ulioanza kutekelezwa mwaka 2012 kwa ufadhili wa pamoja baina ya serikali ya Tanzania, Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Mfuko wa Dunia wa Mazingira (GEF) umejikita katika maeneo makubwa mawili.

Aliyataja maeneo hayo kuwa ni ukanda wa Ruaha unaohusisha Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, maeneo ya jumuiya za hifadhi za wanyamapori ya Mbomipa na Umemarua, na mapori ya akiba ya Rungwa, Muhesi na Kizigo.

Ukanda mwingine kwa mujibu wa mratibu huyo, ni wa Kitulo-Kipengele unaohusisha Hifadhi ya Taifa ya Kitulo, pori la akiba la Mpanga Kipengele, bonde la Numbe, na hifadhi ya mlima Rungwe na Bujingijila.

Katika hifadhi ya Kitulo, Meing’ataki alisema mradi umeshughulikia changamoto zake mbalimbali ikiwemo ya kuboresha usimamizi wa hifadhi hiyo kwa kuweka alama za mipaka yake na kutoa elimu ya uhifadhi na ulinzi kwa wananchi wanaozunguka hifadhi hiyo.

Alisema mbali na kutoa mafunzo kwa askari wa hifadhi, mradi utaiwezesha hifadhi hiyo kufanya ulinzi kwa kutumia mfumo wa mawasiliano wa kidigitali, teknolojia itakayofungwa mwaka huu.


“Lakini pia tumetoa mafunzo kwa askari wa hifadhi na kuongeza vifaa vya ulinzi likiwemo gari kwa ajili ya doria,” alisema na kuongeza kwamba mradi pia umefanya utafiti wa kujua kilichopo katika hifadhi hiyo kwa sasa.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment