Thursday, 9 February 2017

MBUNGE KABATI AFANYA MAKUBWA IRINGA
MBUNGE wa Viti  Maalum  Mkoa  wa  Iringa Ritta Kabati (CCM) ameipiga jeki timu ya wandishi wa habari wa mjini Iringa inayojiweka sawa kushiriki mashindano mbalimbali katika kipindi cha mwaka huu.

Kabati ameipatia timu hiyo seti  moja ya jezi, mpira na pesa taslim kiasi cha Tsh  50O,000 ili viwasaidie katika malengo yao ya kukuza mchezo huo mkoani Iringa.

Pamoja na kutoa msaada huo, mbunge huyo kipenzi wa maendeleo ya wanawake na vijana mkoani Iringa alikubali kuwa mlezi wa timu hiyo kwa kipindi cha maisha yake yote.

Akikabidhi  msaada  huo kwa Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa, Frank Leonard mbunge huyo alisema; “kwanza nakubali kuwa mlezi wa timu hii kwasababu naiona dhamira mliyonayo wanahabari katika kuukuza mchezo huu.”

“Lakini pili ni kwasababu mnataka kuifanya timu yenu kuwa moja ya timu bora za mchezo huu mkoani na katika Taifa kwa ujumla,” alisema.

Kabati alisema mpira ni ajira inayolipa kuliko ajira nyingi duniani wakati akitoa wito kwa vijana kushiriki katika mchezo huo kwa malengo.

Kabati  aliwataka   wadau  wengine mkoa  Iringa na nje ya  Iringa  kuendelea  kujitolea  kuisaidia   timu   hiyo    ya wanahabari ili iendele kufanya vema ndani na nje ya mkoa wa Iringa.

“Niwaahidi pia kuwaombea mechi ya kirafiki na timu ya wabunge na maandalizi yatakapokamilika nitawajulisha,” alisema huku akiwataka waendelee na mazoezi.

Akipokea vifaa hivyo, Leonard alimshukuru mbunge huku akiahidi kusaidia kuisimamia timu hiyo ili ifikie malengo yake.a

Alisema timu hiyo imekuwa ikifanya vema katika mashindano mbalimbali inayoshiriki kwasababu inaundwa na waandishi vijana wenye mwamko wa hali ya juu katika mchezo huo.

“Nawaomba wadau wengine mjitokeze kutuunga mkono, na hivi karibuni tutakuwa na mechi za kirafiki kwa wanahabari majirani zetu wa mikoa ya Mbeya na Morogoro,” alisema.

Hivikaribuni timu hiyo ilitwaa kikombe, Sh 300,000 taslimu na kufanya ziara katika hifadhi ya Taifa ya Ruaha baada ya kuichapa bila huruma timu ya Kitisi FC ya Iringa Vijijini ambayo ni mabingwa wa Kombe la SPANEST, linalofadhiliwa Mradi wa Kuboresha Mtandao wa Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania (SPANEST) na  Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).


Reactions:

0 comments:

Post a Comment