Tuesday, 28 February 2017

CHADEMA YAWEKA ULINZI NYUMBANI KWA MAMA WEMA

Mama-wema

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimedai kuwa kimelazimika kuweka ulinzi katika nyumba ya Mama Mzazi wa Muigizaji wa Bongo Muvi, Wema Sepetu, Mariam Sepetu baada ya kudaiwa kupigwa mawe usiku wa kuamkia jana.

Mawe hayo yanadaiwa kupigwa juu ya bati kwa muda wa saa moja na nusu katika nyumba iliyo maeneo ya Sinza Mori, Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza nyumbani kwake, Mama Sepetu amesema kuwa usiku wote huo alikosa raha na kupata hofu kubwa na kuhisi kuna watu wabaya waliokuwa wanataka kumvamia.

“Nimekosa usingizi na hofu juu huku simu yangu iliishiwa salio kwani nilikuwa nikitaka kupigia simu ndugu na majirani ili waje kunisaidia, sikuweza kutoka nje kwa kuwa sikuwa najua mbaya wangu amekaa wapi na amekusudia kufanya nini,” amekaririwa akisema Mama Wema.

Aidha mama huyo amesema kulivyopambazuka alitoa taarifa kwa mwanae Wema na viongozi wengine wa Chadema ambapo Meya wa Ubungo, Boniface Jacob alifika ili kuangalia hali ya mama huyo na kuamua kumwekea ulinzi.

“Tumeshaangalia mazingira yote tumegundua kitu ambacho hatutakiweka wazi kwa sasa ila tutaweka ulinzi mkali na atakayejaribu shauri yake hatutakubali suala hili liendelee kumkuta kamanda wetu na mimi mara kwa mara nitafika kuangalia mazingira,” amesema Jacob.


Hivi karibuni Wema alitangaza kukihama Chama Tawala CCM na kuhamia Chadema na kukabidhiwa kadi ya chama hicho mbele ya waandishi wa habari akiwa ameongozana na mama yake.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment