Sunday, 15 January 2017

WAWEKEZAJI WATAKA MFUMO WA KUKUSANYA VAT UANGALIWE UPYA


KAMPUNI ya Green Resources Ltd (GRL) kupitia kampuni yake dada ya kiwanda cha Saohill cha mjini Mafinga mkoani Iringa imeomba mfumo wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wa ukusanyaji kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) uangaliwe upya kwani unahatarisha mtaji na uhai wa kampuni yao.

Taarifa hiyo ilitolewa juzi na Meneja wa Kiwanda cha Saohill Viatus Bahati kwa  Naibu Waziri wa Kazi, Vijana na Ajira, Antony Mavunde aliyeitembelea kampuni hiyo kujionea jinsi inavyotekeleza sheria ya ajira na mahusiano kazini.

Wakati GRL inajishughulisha na upandaji miti katika wilaya za Mufindi na Kilombero, ikiwa imekwishapanda zaidi ya hekta 17,000 za miti katika wilaya hizo; kiwanda chake cha Saohill kijishughulisha na utengenezaji wa nguzo na bidhaa zingine zitokanazo na mbao.

Bahati alimwambia waziri huyo kwamba kampuni yao ina mkataba wa kusambaza nguzo za umeme kwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa muda mrefu na ni wakala wa TRA wa ukusanyaji wa kodi hiyo.

Akizungumzia mchakato wa utengenezaji wa nguzo hizo na usambazaji wake kwa shirika hilo, alisema umekuwa ukichukua siku 180 hadi kupata malipo yake.

“Hatua ya kwanza ambayo huchukua siku 90 hutumika kuandaa nguzo hizo kiwandani, na hatua ya pili inahusisha kusambaza nguzo hizo kwa shirika hilo pamoja na hati yake ya madai,” alisema.

Alisema wakati Tanesco wamekuwa wakichukua zaidi ya siku 90 kulipa fedha zao na za kodi hiyo, kwa sheria hiyo ya TRA wanatakiwa kulipa kodi hiyo ndani ya siku 28 jambo linalowazimu kufanya malipo hayo kwa kutumia fedha zao za mtaji.

“Kila tunaposambaza nguzo kwa shirika hilo, tunajikuta tunalazimika kumega sehemu ya mtaji ili kulipa VAT ya bidhaa ambazo hatujalipwa,” alisema.

Alisema utekelezaji wa sheria hiyo unaiyumbisha kampuni yao kimtaji, kiuendeshaji na maendeleo yake jambo lililosababisha sehemu kubwa ya wafanyakazi wake wapunguzwe kazi.

“Kampuni ilikuwa na wafanyakazi 575, lakini kwa kuzingatia mazingira ya sasa Desemba mwaka jana tulipunguza wafanyakazi 190 kwa mara moja,” alisema Bahati.

Bahati alimuomba Mavunde alifikishe ombi lao serikalini ili sheria hiyo iweze kuangaliwa upya kwa maslai mapana yatakayoendeleza viwanda nchini.

Mavunde alifika kiwandani hapa baada ya kuwepo kwa taarifa kwamba kampuni hiyo haitekelezi baadhi ya vipengele vya sheria hiyo kama inavyotakiwa.

Wakizungumza na waziri huyo, baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo walisema hawana mikataba ya ajira pamoja na kufanya kazi kwa muda mrefu, na wamekuwa wakitumikishwa kama vibarua.

Malalamiko mengine yaliyotolewa na wafanyakazi hao ni pamoja na kupunjwa malipo yao ya nauli ya likizo, wanatishwa kujiunga na vyama vya wafanyakazi, wanafanya kazi zaidi ya saa 45 kwa wiki, na malipo yao kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii ni ya kusuasua.

Mavunde aliiagiza kampuni hiyo kurekebisha mapungufu yote yanahusu sheria za kazi huku akiwaagiza wasaidizi wake kufuatilia kwa karibu utekelezaji wake baada ya kuwapa wafanyakazi hao namba zake za simu watakazotumia kumpa taarifa kama mapungufu yaliyotajwa yataendelea kuwepo.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment