Sunday, 29 January 2017

WANAOKOPESHA FEDHA KWA RIBA MITAANI KUKAMATWA..


SERIKALI imetangaza kuwasaka na kuwafikisha katika vyombo vya dola wafanyabiashara wa mitaani wanaokopesha fedha kwa riba bila kuwa na leseni ya biashara hiyo.

Pamoja na wafanyabiashara hao, Waziri wa Katiba na Sheria Dk Harrison Mwakyembe ameomba wananchi wasaidie kuwafichua askari Polisi na mahakimu wanaowapa nguvu wafanyabiashara hao kinyume na sheria.

Akizungumza na wanahabari jana mjini Iringa, Dk Mwakyembe alisema; “Baada ya kuwasilia mjini Iringa jana (juzi) kikazi, nilifuatwa na akina mama watano waliowalalamikia watu binafsi wenye fedha wanaofanya biashara hiyo.”

Bila kuwataja majina, waziri huyo alisema akina mama hao walilalamika kutozwa riba ya hadi asilimia 240 kwa mikopo wanayochukua jambo linalowatia umasikini kwa kuwafanya wawe watu wa kudaiwa katika maisha yao yote.

Dk Mwakyembe alisema kwa mujibu wa sheria namba 5 ya 2006 ni kosa la jinai kwa mtu yoyote yoyote kufanya biashara ya kukopesha fedha bila kuwa na leseni ya biashara hiyo inayotakiwa kulipiwa kodi.

“Baada ya kufikishwa mahakamani na kupatikana na hatia, adhabu kwa mtu anayepatikana na kosa hilo ni ama kifungo cha miaka mitano jela au faini ya Sh Milioni 20,” alisema.

Wakati sheria hiyo ikiwa wazi, alisema amepokea taarifa kutoka kwa akina mama hao kwamba wapo baadhi ya askari Polisi wa mjini Iringa kwasababu wasizozifahamu wamekuwa wakizifanya kesi zinazohusu mikopo hiyo kuwa za jinai badala ya madai.

“Pamoja na askari hao kuna mahakimu, wanaoshirikiana na wafanyabiashara hao kutengeneza mikataba ya mikopo hiyo na kusimamia kesi zake pale, waombaji wa mikopo wanaposhindwa kulipa,” alisema.

Alisema kwa nguvu ya askari na mahakimu hao, wanaoshindwa kulipa mikopo hiyo hunyang’anywa mali zao na watu wenye benki hizo alizoziita benki kanjanja na kuuzwa kwa watu wengine jambo linalozidisha umasikini kwa wajasiriamali hasa wanawake.

“Haya ndiyo yanayotokea hapa Iringa, na yanaweza kuwa yanatokea sehemu nyingine nchini, kuna watu wanajifanya benki, wanapanga kuwaibia watu kupitia mikopo yao huku wakijua huwezi kukopesha watu bila kuwa na leseni na kulipa kodi,” alisema.

Akishtushwa na taarifa hizo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alisema hazijawahi kufikishwa ofisini kwake na akaitumia taarifa hiyo ya waziri kutoa maelekezo ya kuzishughulikia.

“Namuagiza mkuu wa wilaya ya Iringa, kesho Jumatatu, saa nne asubuhi akutane na wananchi wote wenye malalamiko hayo katika Jumba la Maendeleo, mjini Iringa,” alisema.

Akiwaomba wananchi hao watoe ushirikiano, Masenza alisema zikipatikana, taarifa hizo zitawawezesha kuchukua hatua stahiki kwa wale wanaohusika.

“Pia ipo sheria inayonipa nafasi mimi kama mkuu wa mkoa kwa kupitia kamati ya mahakama kuwajadili mahakimu wa mahakama za mwanzo na kwa msaada wa hakimu mkazi mfawidhi wa mkoa kutoa hukumu kwa mahakimu hao,” alisema

Reactions:

0 comments:

Post a Comment