Sunday, 29 January 2017

WANAOKOPESHA FEDHA BILA LESENI IRINGA KUSHITAKIWA KESHO


MKUU wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela kukutana na wananchi wenye malalamiko yanayowahusu watu wanaofanya biashara ya kukopesha fedha mitaani bila ya kuwa na leseni.

“Namuagiza mkuu wa wilaya ya Iringa, kesho Jumatatu, saa nne asubuhi akutane na wananchi wote wenye malalamiko hayo katika Jumba la Maendeleo, mjini Iringa,” alisema wakati akiahidi kutekeleza agizo lililotolewa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe kuhusu wafanyabiashara hao.

Dk Mwakyembe alisema wafanyabiashara hao wanavunja sheria namba 5 ya mwaka 2006 inayowazuia watu wasio na leseni kufanya biashara ya kukopesha fedha kwa riba huku wakiikosesha serikali mapato yake stahiki kwa njia ya kodi.

“Adhabu kwa mtu anayepatikana na kosa hilo ni ama kifungo cha miaka mitano jela au faini ya Sh Milioni 20,” alisema.

Alisema anazo taarifa zinazohusu uwepo wa wafanyabiashara hao mjini Iringa, wanaopora mali za watu wanaoshindwa kulipa mikopo yao kwa nguvu ya baadhi ya askari Polisi na Mahakimu.

Waziri huyo alisema wanaokopeshwa na wafanyabiashara hao wa benki kanjanja wanalalamika kutozwa riba ya hadi asilimia 240 kwa mikopo wanayochukua jambo linalowatia umasikini kwa kuwafanya wawe watu wa kudaiwa katika maisha yao yote.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment