Monday, 9 January 2017

WADAU HIFADHI YA RUAHA, WAOMBA BARABARA YA LAMI

WADAU wa sekta ya utalii nchini wamempigia magoti Rais Dk John Magufuli wakimuomba aiunganishe hifadhi ya Taifa ya Ruaha na mtandao wa barabara ya lami ili kuongeza kasi ya kuikuza sekta hiyo katika mikoa ya kusini na uchumi.

Hifadhi ya Taifa ya Ruaha ndiyo kubwa kuliko zote Tanzania, na ni ya pili kwa ukubwa barani Afrika baada ya hifadhi ya Kafue ya nchini Zambia.

Hifadhi hiyo inayozungukwa na mikoa ya Iringa, Mbeya, Songwe na Dodoma katika wilaya ya Iringa, Mbarali, Mufindi, Chunya na Chamwino ina malango mawili ya kuingilia.

Lango kuu kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kaimu mhifadhi mkuu wa hifadhi hiyo, Moronda Moronda ni barabara ya kilometa 128 toka Iringa Mjini na lango la Ikonga, wilayani Mbarali mkoani Mbeya.

Akizungumza na wanahabari hivikaribuni, Moronda alisema ni kero kwa watalii, madereva na vyombo vya usafiri vinavyotumia barabara hizo kwasababu hali yake ni mbaya.

“Barabara ya Iringa hadi hifadhini ni balaa na hali hiyo kwa sehemu yake imekuwa ikipunguza kasi ya ukuaji wa sekta hii ya utalii,” alisema na kuomba serikali ya awamu ya tano ifanye maamuzi yatakayowezesha barabara hiyo kujengwa kwa kiwango cha lami kwa kuzingatia mahitaji ya sasa. 


Kwa upande wake Afisa wa Mradi wa Kuboresha Mtandao wa Maeneo ya Hifadhi Kusini mwa Tanzania (SPANEST), Malima Mbigima alisema Tanzania bado haijaanza kunufaika na uwepo wa hifadhi hiyo kubwa nchini.

Alisema miundombinu ikiboreshwa kwa kiwango kinachoombwa na wadau, sekta ya utalii kusini mwa Tanzania italeta faida kubwa ikiwemo kuongezeka kwa pato la Taifa.

“Mapato katika sekta hii yataongezeka kwa vivutio vyetu kutembelewa na wageni wengi zaidi wa ndani na nje ya nchi,” alisema.

Kwa mazingira ya sasa, Mbigima alisema sio rahisi sana kuona watu wa kawaida wakitembelea hifadhi hiyo na nyingine kwa kutumia magari yao kwa hofu ya kuharibika kutokana na ubovu wa miundombinu ya barabara.

Pamoja na ubovu wa miundombinu ya barabara, aliiomba serikali kuendelea kushirikiana na sekta binafsi ili ijenge hoteli za kutosha na zenye ubora wa kitaifa na kimataifa ili zipokee wageni wenye hadhi tofauti.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment