Tuesday, 17 January 2017

TUCTA KUCHUNGUZA MKATABA WA UJENZI WA JENGO HILI JIJINI MBEYA

Tokeo la picha la kabwe mbeya


UONGOZI mpya wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) umetangaza kufanya mapitio ya mkataba wa jengo la kitega uchumi lililojengwa katika eneo lake  la Chuo cha Wafanyakazi jijini Mbeya (Kabwe, Mwanjelwa).

Pamoja na kupitia mkataba huo, uongozi huo umesema utafanya uhakiki na tathmini ya mali zake zote nchini ili kuona kama zinatumika kwa maslai ya wanachama wa vyama vya wafanyakazi na kuchukua hatua za haraka itakapobainika hali ni tofauti.

Taarifa hiyo ilitolewa jana mjini Iringa na Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamghokya wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO).

“Baada ya wiki mbili toka leo, tutakuwa jijini Mbeya kuona jinsi uongozi wa chuo ulivyoingia mkataba na wafanyabiashara waliojenga jengo hilo kubwa la biashara la ghorofa moja,” alisema .

Alisema taarifa za awali zinaonesha kuwepo kwa mkataba aliouita wa ovyo kwa madai kwamba TUCTA ambao ni wamiliki wa chuo hicho, wanalipwa Sh 20,000 tu kwa mwezi kwa kila chumba cha biashara katika jengo hilo.

Nyamghokya alisema kwa kupitia mkataba huo; “taarifa zinaonesha wafanyabiashara hao wataendelea kulipa kiasi hicho cha kodi kwa kipindi cha kati ya miaka 50 na 80, tangu waanze kulitumia jengo hilo miaka mitano iliyopita.”

Huku kukiwepo na mkataba huo, taarifa nyingine iliyotolewa na Katibu wa TUICO wa Nyanda za Juu Kusini, Merboth Kapinga imesema hali ya chuo hicho ni mbaya na kimefika hatua kinaonekana kama hakina mwenyewe.

Kapinga alisema katika mazingira hayo TUICO imejikuta ikilazimika kuchangia gharama za kulipa wafanyakazi wa chuo hicho.

“Tunaomba TUICO ibebe jukumu lake la kukiendeleza na kukiendesha chuo hicho, kwasasa ni kama hakina mwenyewe,” alisema.

Akijibu ombi la Kapinga, Rais wa TUCTA aliahidi kukirudisha chuo hicho kwenye mstari wake ili kifanye kazi kinayotakiwa kufanya kwa maslai ya wafanyakazi wote nchini.

“Siku si nyingi kutakuwa na mabadiliko makubwa katika chuo hicho, tutaboresha menejimenti yake na kuyafanyia kazi mapungufu yake mbalimbali,” alisema.

Akizungumzia mali zingine za TUCTA katika maeneo mbalimbali nchini, Nyamghokya alisema; “TUCTA ina majengo yake kila mkoa na katika maeneo mengine ina viwanja vinavyohitaji kuendelezwa.”

Alisema mali zote hizo zinarudishwa mikononi mwa TUCTA ili zitumike kwa manufaa ya shirikisho, hatua itakayowaondoa kwenye utaratibu ulioanza kuzoeleka wa kuombaomba kwa wafadhili ili kuendesha mambo yao.

“Zipo taarifa kwamba katika baadhi ya majengo ya TUCTA kuna watu wanakaa bure, hawalipi chochote, hiyo sio sawa hata kidogo,” alisema.

Akizungumzia maslai ya wafanyakazi, alisema TUCTA itashirikiana kikamilifu na vyama wanachama kuwatetea pale vyama hivyo vitakapohitaji nguvu yao

Reactions:

0 comments:

Post a Comment