Wednesday, 4 January 2017

RUNGU LA NHC LATUA KWA VITUS MUSHI, NEW AMBASSADOR LODGE & RESTAURANTWIKI nne tangu limuondoe aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa, Chiku Abwao (CHADEMA) katika moja ya nyumba zake za mjini Iringa, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) leo limeendeleza msuri huo kwa kumshughulikia kada maarufu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Vitus Mushi.

Mushi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wakandarasi Mkoa wa Iringa alikuwa mpangaji wa shirika hilo katika jengo la ghorofa moja lililopo kwenye kiwanja Namba 12/2 katika mtaa wa Haile Sellasie, kata ya Gangilonga mjini Iringa, kabla ya kuondolewa jana.

Ndani ya CCM, Mushi amewahi kuwa mjumbe wa vikao vya ngazi mbalimbali za chama hicho na Diwani wa kata ya Mtwivilla mjini Iringa.

Kwa upande wake, Abwao alikuwa mpangaji wa jengo lenye Club maarufu ya VIP lililopo Plot Na 36 katika mtaa huo huo baada ya kukiuka masharti ya mkataba kwa kumpangisha jengo hilo mtu mwingine na kujipatia mamilioni ya shilingi.

HabariLeo ilishuhudia madalali wa kampuni ya udalali ya Majembe wakiondoa vifaa mbalimbali vilivyokuwa vikitumiwa na Mushi kuendeshea biashara ya hoteli na nyumba ya kulala wageni katika jengo hilo.

Akizungumza na wanahabari wakati zoezi hilo likiendelea, Meneja wa NHC Mkoa wa Iringa, Repson Yosiah alisema; “tumefanya oparesheni hii kama manavyoona, huu ni utaratibu wa kawaida na unaoeleweka hasa kwa wateja wasumbufu kulipa kodi.”

Alisema wamemvumilia kwa muda mrefu Mushi anayelitumia jengo hilo kuendesha New Ambassador Lodge and Restaurant kabla ya kuamua kufuata utaratibu wa kisheria wa kumuondoa.

“Mpaka sasa tunamdai karibu Sh Milioni 6 ambayo ni malimbikizo ya kodi ya pango la toka mwezi Agosti hadi Desemba mwaka jana na alipewa tarehe ya ukomo wa kumaliza deni hilo lakini ameshindwa,” alisema.

Endapo atalipa deni hilo baada ya hatua hiyo, Yosiah alisema kama atataka kuendelea kuwa mpangaji wake, Mushi atalazimika kuanza upya mchakato wa kuomba tena kuwa mpangaji katika jengo hilo.

Mushi mwenyewe hakuweza kupatikana kuzungumzia hatua zilizochukuliwa na NHC na maelezo yaliyotolewa na meneja wake Emanuel Maro yanaonesha alikuwa amerejea muda fupi toka safarini.

Akilalamika kutoridhishwa na uamuzi wa kuondolewa katika jengo hilo, Maro alikiri shirika hilo kuwadai huku akisema kiasi kikubwa cha deni hilo ambalo hakulitaja, wamekwishalipa.

“Tunadaiwa miezi mitatu tu hivi sasa, tulikuwa na deni kubwa tukapewa muda wa kulipa na tukapunguza kiasi kikubwa na kubaki kiasi kidogo ambacho tungeweza kulipa ndani ya siku tatu.” Alisema.

Alisema hatua ya NHC ya kuwaondoa ghafla katika jengo hilo kumeathiri biashara yao kwa kiasi kikubwa na hawajui ni kwa namna gani watawafidia wateja wao hasa wale waliokuwa wamepanga kwa siku nyingi katika nyumba ya kulala wageni ndani ya jengo hilo.

Mwakilishi wa kampuni ya udalali ya Majembe, Riziki Kigalo alisema; “tumepewa kazi na NHC, tunatoa vitu vyote na kwenda kuvifungia stoo na tutalifunga jengo hili mpaka atakapomalizana na NHC.”

Jitihada za wajumbe wa serikali ya mtaa huo kuwaomba NHC kuvuta subiora mpaka Mushi atakapolipa deni hilo hazikuzaa matunda.

“Huyo ni mwananchi katika mtaa wetu, anafanya biashara ambayo ina manufaa makubwa sio tu kwa wakazi wa mtaa huu, lakini kwa watu wengi wa ndani na nje ya mkoa, lakini pia ametoa ajira hapa, kwa maamuzi haya ya NHC athari ni kubwa,” alisema Alli Yakuti mjumbe wa mtaa huo.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment