Monday, 9 January 2017

IRINGA WAHAMASISHWA KUFUGA SUNGURA KIBIASHARA

 


ALIYEKUWA Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa na Mwenyekiti wa Bunge lililopita, Lediana Mng’ong’o amewataka vijana na wanawake kuitumia fursa ya ufugaji wa sungura kibiashara wakati akiwasihi waache malalamiko ya ukosefu wa hela mifukoni (ukata).

Aliyasema hayo leo kwenye mafunzo ya siku moja ya uzalishaji wa sungura kibiashara yaliyotolewa kwa wajasiriamali mbalimbali wa mjini Iringa na Tanzania Business Creation Company Ltd (TBCC).

“Ule muda wa kufanya vitu kwa mazoea umepitwa na wakati; hu ni muda wa kutumia fursa mpya za ajira kujiongezea kipato na moja ya fursa hiyo mpya ni hii tunayoelezwa hapa leo ya ufugaji wa sungura kibiashara,” alisema.

Alisema mahitaji ya nyama ya sungura ndani na nje ya nchi ni makubwa huku kiwango kinachozalishwa hivisasa kikishindwa kumudu soko hilo kwa kuwa ni kidogo.

“Tubadilishe mitizamo, tuache kufanya zile shughuli tulizozizoea ambazo hazituletei mabadiliko na badala yake tuingie kwenye fursa hizi mpya,” alisema huku akiahidi pia kuingia katika shughuli ya ufugaji wa Sungura hao.

Ili kuwafanya wafugaji wa sungura wafurahie ufugaji huo, mkufunzi wa TBCC, Selemani Boko alisema kampuni yao inatoa mafunzo ya mara kwa mara, inawatembelea na kuwakutanisha na wataalamu wa afya ya mifugo ili kuwapa ushauri Zaidi

“Kwa anayetaka kuingia katika uzalishaji huu atambue kuwa hii ni shughuli kubwa ya kiuchumi (biashara) yenye soko kubwa ndani na nje ya nchi ambalo kwa kiasi kikubwa bado halijafikiwa,” alisema.

Alisema kwasasa kampuni yao inahitaji Sungura 18,000 kwa mwezi kwa ajili ya soko la ndani huku mahitaji ya soko la nje yakiwa kati ya tani 70 hadi 150 kwa kipindi hicho.

“Kwa soko la ndani bado hatujafikia hata nusu ya mahitaji na ukienda soko la nje tumeshindwa kusaini mikabata iliyopo mezani ya usambazaji wa sungura hao kwasababu hawapo,” alisema.

Alisema nyama ya sungura ni lishe bora inayohimizwa matumizi yake kwa watanzania wote kwani ni nyeupe isiyo na mafuta ya lehemu (cholesterol).

 “Kwa anayetaka kufuga tunampatia mafunzo, banda la kufugia, sungura wa mbegu, madawa, vyakula vya sungura chini ya uangalizi na uratibu; na tunaingia mkataba wa kununua sungura wote wanaozalishwa kipindi wanapofika umri wa kuuzwa,” alisema.

Alisema mfugaji hana sababu ya kutokufuga kwa kuhofia soko kwani soko lipo kwao na kwa wastani Sungura aliyetunzwa vizuri huwa na uzito wa kilo 4 hadi 5 na kampuni hununua kilo moja kwa Sh 8,000.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment