Monday, 19 December 2016

WANAHABARI IRINGA FC WAIGARAGAZA KITISI FC
Mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela timu inayozidi kuimarika ya Wanahabari FC ya mjini Iringa, imewafunga mabingwa wa kombe la SPANEST, Kitisi FC kwa mikwaju ya penati 5-4.

Timu hizo ziliingia hatua ya matuta baada ya kumaliza dakika 90 za mchezo huo wa hisani  uliopigwa katika uwanja wa Lyambangali, ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, kwa sare ya 1-1.

Kwa ushindi wa mchezo huo wa hisani, Wanahabari FC imetwaa kikombe na Sh 300,000 taslimu; zawadi walizokabidhiwa na mkuu wa wilaya huyo aliyeahidi kuisaidia timu hiyo.

Mchezo huo ulioratibuwa na Mradi wa Kuboresha Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania (SPANEST), huzikutanisha bingwa wa Kombe la SPANEST na timu yoyote kutoka katika ukanda huo kama moja ya zawadi kwa mabingwa wa kombe hilo.

Kwa kupitia mchezo huo, timu hizo hupata fursa ya kufanya utalii wa ndani kwa kutembelea vivutio mbalimbali ndani ya hifadhi hiyo ya Taifa ya Ruaha.

Kitisi FC ambayo haikutarajia kuupoteza mchezo huo huku ikiwa na kumbukumbuku ya kutwaa ubingwa wa kombe la SPANEST wiki tatu zilizopita, iliondoka na zawadi ya Sh 200,000 kama kifuta machozi.

Ikitwa Kombe la SPANEST baada ya kuifunga Kinyika FC kwa mikwaju ya penati 4-2, Kitisi iliondoka na na kombe, medali za dhahabu, seti moja ya jezi, cheti na Sh Milioni moja taslimu.

Mratibu wa SPANEST inayoratibu mashindano hayo, Godwell Ole Meing’ataki alisema kwa pamoja kombe la SPANEST na mchezo huo wa hisani unalenga kuwahamasisha vijana kuoa Tembo kwa kupitia kauli mbiu yake ya “Piga Vita Ujangili, Piga Mpira Okoa Tembo.”

Meing’ataki alisema wazo la kuunganisha vijana katika vita ya ujangili linaonekana kuwa njia muafaka ya kutokomeza ujangili kutokana na ukweli kwamba vijana ndiyo walengwa wakubwa katika kushawishika kuingia kwenye maeneo yaliyohifadhiwa na kufanya ujangili.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment