Friday, 16 December 2016

WAKULIMA IRINGA WAITUHUMU BENKI YA MAENDELEO YA KILIMO

VYAMA vya ushirika vya msingi 10 vya mkoani Iringa vimeazimia kuishitaki kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) vikiituhumu kwa urasimu wa utoaji mikopo ya pembejeo wakati msimu huu wa kilimo ukiwa umeanza.

Wakizungumza na wanahabari mjini Iringa jana, wawakilishi wa vyama hivyo ambavyo ni wanachama wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Iringa (IFCU) walisema pamoja na kutekeleza masharti muhimu ya kupata mikopo hiyo hadi sasa hakuna kati yao aliyepata mikopo waliyoomba.

Wakati ikizindua rasmi shughuli zake katika hafla ya utoaji wa mikopo iliyofanyika katika kijiji cha Igomaa, wilayani Mufindi mkoani Iringa Januari mwaka huu, Mkurugenzi wa Mikopo na Biashara wa benki hiyo Robert Pascal alitaja vigezo wanavyozingatia katika utoaji wa mikopo kuwa:

“Ni pamoja na vikundi hivyo kuwa na taarifa za akaunti za benki, barua za maombi, usajili wa kikundi, mtiririko wa mapato na matumizi, andiko la biashara,  katiba, cheti cha ukomo wa madeni, taarifa za ukaguzi wa fedha na dhamana za mikopo.

Mwenyekiti wa IFCU, Felix Nyenza alisema vyama hivyo vyenye wanachama zaidi ya 900 viliomba zaidi ya Sh Milioni 500 kwa ajili ya msimu huo wa kilimo kupitia mchakato ulioanza Agosti mwaka huu.

“Toka wakati huo, kumekuwa na nenda, rudi, lete hiki, bado kile hatua iliyowakatisha tamaa wakulima hawa waliomini benki hii haina urasimu na masharti yake yanaweza kuleta nafuu na kuongeza tija kwa mkulima,” alisema.

Nyenza alisema benki hiyo inataka kusababisha kilio kwa vyama hivyo ambavyo kabla ya benki hiyo kuanza kufanya kazi yake, vilikuwa vikipata mikopo ya kilimo kutoka katika taasisi zingine za fedha.

Kwa kupitia mikopo hiyo, Nyenza alisema matarajio ya wakulima hao ilikuwa ni kupata kwa wakati pembejeo za uhakika zikiwemo mbegu bora, mbolea na dawa, vifaa na fedha kwa ajili ya kulipia gharama mbalimbali za uzalishaji.

Alisema wakati msimu wa kilimo umekwishaanza, wakulima wanashindwa kuandaa mashamba yao kwa kiwango walichotarajia, hawana pembejeo na hawajui kama watapata mahitaji mengine ili kuongeza tija katika shughuli hiyo.

Alisema vyama hivyo vimetumia zaidi ya Sh Milioni 10 katika mchakato wa kuomba mikopo hiyo na huku wakishindwa kuelewa nini kitatokea, wamekuwa wakipata mawasiliano ya shida na maafisa wa benki hiyo walioko Dar es Salaam.

Awali Katibu wa Chama cha Msingi cha Utoleta (Utoleta Amcos Ltd), Victor Mwipopo alisema; “kwa kadri siku zinavyokwenda ushirikiano na benki unazidi kuwa mdogo, hatuelewi, tatizo ni nini au benki haikujipanga vizuri?” 


Naye  Abu Chang’a wa Chama cha Msingi cha Kiwele alisema imani kwa benki hiyo waliyoitumia kushawishi wanachama wenzao kuacha kukopa kwenye taasisi walizozizoea inaweza kuwaongezea umasikini kama watakosa mikopo hiyo.

“Tumekubaliana endapo tutakosa mikopo hiyo, tutakwenda kuishitaki benki hiyo kwa Waziri Mkuu,” alisema Asheri Lupembe ambaye ni katibu wa Chama cha Ushirika Nyeyembe (Nyenyembe Amcos) cha Malangali, Mufindi.

Wakati vyama hivyo vikiilalamika benki hiyo, Januari mwaka huu, benki hiyo ilizindua huduma zake na kutoa mikopo ya zaidi ya Sh Bilioni 1 kwa vikundi nane vya wakulima wa mahindi na mpunga vya mkoa wa Iringa.

Vikundi hivyo na kiasi cha fedha walichopata ni Idodi Farmers Association chenye wakulima 108 (Sh milioni 119.3), Igomaa Cooperative Society chenye wakulima 130 (Sh Milioni 180.4), na Kihorogota Cooperative Society wakulima 85 (Sh Milioni 77.4).

Vingine ni Kilolo Mali Mbichi Amcosi wakulima 31 (Sh Milioni 53.4), Mgololo Cooperative Society wakulima 87 (Sh Milioni 132), Mtambula Amcosi  wakulima 160 (Sh Milioni 69), Mufindi Cooperative Society wakulima 152 ( Sh Milioni 221) na usolanga Cooperative Society wakulima 104 (Sh Milioni 124.1).

Reactions:

0 comments:

Post a Comment