Thursday, 1 December 2016

SAKATA LA VIWANJA VYA IGUMBILO LAIBUKA TENA, MWENYEKITI ATAKA KATIBU WAKE ASIMAMISHWE
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Iringa kimeliibua upya suala la uuzaji wa baadhi ya viwanja vya Igumbilo vya mjini Iringa, mali ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), kikitaka viongozi watendaji wa chama wanaotuhumiwa kuhusika na kashfa hiyo kusimamishwa uongozi.

Pamoja na kutaka viongozi hao kusimamishwa ili kupisha uchunguzi huru wa kashfa hiyo ya zaidi ya mwaka mmoja sasa, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Dk Jesca Msambatavangu aliwataka waliouziwa viwanja hivyo kutoviendeleza mpaka mgogoro dhidi ya viwanja hivyo vinavyodaiwa kuuzwa kinyemela utakapokwisha.

Taarifa ya UVCCM iliyotolewa na Katibu wa UVCCM Mkoa wa Iringa, Abdukarim Alamga inaonesha UVCCM ilikuwa na shamba la zaidi ya heka 210 zilizopimwa ili kukidhi sheria za mipango miji na kupata viwanja zaidi ya 150.

Alamga alisema UVCCM ngazi ya Taifa inaendelea kulitafutia ufumbuzi kashya ya uuzaji wa baadhi ya viwanja hivyo na kwamba hivi karibuni Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Shakha Mamdu Shaka alikuwepo mjini Iringa na kufanya majadiliano ya siri na baadhi ya watu waliouziwa.

Akizungumza na wanahabari katika viwanja hivyo Dk Msambatavangu alisema kumekuwepo na taarifa zinazomtaja Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga na Katibu wa CCM Manispaa ya Iringa, Elisha Mwampashi kuhusika katika kashfa hiyo.

“Watendaji hao wanatajwa katika kashfa hii, na mimi kama msimamizi mkuu wa shughuli za chama mkoani hapa nitafuatilia suala la watendaji hao; ili wasivuruge uchunguzi wanatakiwa kusimamishwa kazi,” alisema.

Alimpongezea Rais Dk John Magufuli kwa kutumbua majipu na kuwasimamisha kazi baadhi ya watumishi wanaotuhumiwa kwa vitendo vya ufisadi na rushwa na akasema hatua kama hizo zinatakiwa kuchukuliwa pia ndani ya chama.

Alisema ataandika barua makao makuu ya chama hicho ili kuomba watendaji hao wasimashwe kazi mpaka mgogoro huu utakapokwisha na kama itabainika hawahusiki na tuhuma hiyo basi watarudishwa kazini kama taratibu zinavyotaka.

Wakati hayo yote yakiendelea, aliwaagiza wenyeviti wa UVCCM Manispaa ya Iringa na Iringa Vijijini kuhakikisha wanashirikisha vijana wao kulilinda eneo hilo mpaka pale mgogoro huo utakapokwisha.

“Naomba waliouziwa viwanja katika eneo hili wawe na subira. CCM ni chama cha haki na ni imani yangu katika hili kitatenda haki pia,” alisema.

Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa, Mtenga alikanusha kuhusika katika tuhuma hizo akisema UVCCM inaendeshwa kwa katiba yake ambayo yeye kama mtendaji wa chama hana mamlaka ya kuingilia.

“Katika nyaraka zote zinazohusiana na uuzaji wa viwanja hivyo, hakuna mahali ambapo mimi kama Mtenga natajwa kuhusika kwenye maamuzi yake, yawe yalifuata utaratibu au hayakufuatwa utaribu,” alisema.

Alisema moja ya hatua aliyochukua baada ya kusikika taarifa za uuzaji tata wa baadhi ya viwanja hivyo aliandikia barua katika ofisi ya Mkurugenzi ya Manispaa ya Iringa akiitaka isitoe hati za viwanja kwa watu waliouziwa kinyemela.

Alisema hakuna mali ya chama hicho inaweza kuuzwa pasipo kuridhiwa na Baraza la Wadhamini wa chama kwahiyo kama kuna mtu aliuziwa kinyume na utaratibu huo amtafute aliyemuuzia ili amdai fedha zake.

Mtenga alisema kwa kupitia msingi huo ndio maana kashafa hiyo ilipofikishwa kwenye vyombo vyo dola hakuwa mmoja wa waliofikishwa mahakamani kabla kesi hiyo haijafutwa.

Mei mwaka huu, Katibu wa CCM Manispaa ya Iringa, Elisha Mwampashi na aliyekuwa Katibu wa UVCCM Mkoa wa Iringa, Alli Nyawenga walitiwa mbaroni na kufikishwa mahakamani mjini Iringa wakituhumiwa kuhusika na uuzaji wa viwanja hivyo.

Baada ya wawili hao kukamatwa, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, John Kauga alizungumza na wanahabari na kusema kwamba viongozi walikamatwa baada ya kushitakiwa na Tume ya Uchunguzi ya Baraza la Wadhamini la UVCCM Taifa.

Alisema taarifa za uchunguzi wa awali wa jeshi hilo zilionesha watuhumiwa hao kuhusika na uuzaji wa viwanja hivyo kati ya Machi na Desemba mwaka jana.

Oktoba mwaka huu, kesi hiyo ilifutwa kwa kile kilichodaiwa kupisha uchunguzi zaidi wa kashfa hiyo iliyomuondoa madarakani Nyawenga huku Mwampashi akirudishwa kwa maelekezo ya chama kuendelea na majukumu yake ya ukatibu.

Taarifa iliyotolewa jana na Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa inaonesha mapema wiki hii, Mwampashi amepata uhamisho unaompeleka mkoani Dodoma atakakokuwa Katibu wa CCM Manispaa ya Dodoma.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment