Sunday, 11 December 2016

MWEKEZAJI ACHEPUSHA MAJI MBARALI, APEWA ONYO KALIOFISI ya Maji ya Bonde la Rufiji imetoa onyo kali kwa Kampuni ya Highlands Estate inayojishughulisha na kilimo cha mpunga wilayani Mbarali, mkoani Mbeya baada ya kuchepusha maji ya mto Balali hatua iliyoathiri mtiririko wa maji katika Mto Ruaha unaomwaga maji yake katika Mto Ruaha Mkuu.


Taarifa za kuchepusha maji hayo zilitolewa na wananchi wa kata ya Imalosongw, Ubaruku kuliko na mashamba makubwa ya kampuni hiyo waliokuwa wakilalamika kukosa maji kwa matumizi ya majumbani, mifugo na shughuli zao za kilimo baada ya tukio hilo.

BONGO LEAKS iliyotembelea eneo hilo hivikaribuni, ilishuhudia sehemu kubwa ya mto Ruaha unaotiririsha maji kuelekea Mto Ruaha Mkuu kwa kupitia bonde la Ihefu, ikiwa imekauka.

Ofisa wa Maji wa Bodi ya Maji ya Bonde la Rufiji, Idris Msuya alisema baada ya kusikia malalamiko ya wananchi hao, aliwaagiza maafisa wa Bonde la Rufiji kufanya uchunguzi.

Alisema katika uchunguzi wao walibaini taarifa za wananchi zina ukweli na kumuagiza mwekezaji huyo kufungua maji hayo huku akipewa onyo kali.

Alisema kampuni hiyo ilichepusha maji hayo ili kufanikisha maandalizi ya upandaji wa mbegu za mpunga kwa ajili ya mashamba yake.

Msuya alisema wamempa onyo kali na endapo atarudia kufanya kosa kama hilo au lolote kinyume na masharti ya kibali chake cha matumizi ya maji watamchukulia hatua kazi zaidi.

Akizungumzia sheria ya usimamizi wa rasilimali za maji, Msuya alisema Bodi ya Maji ya Bonde inaweza kutoa kibali cha kuchepusha, kukinga, kutunza, kuchukua na kutumia Maji kutoka chanzo cha maji kwa kutaja kiasi cha maji yatakayochukuliwa, matumizi yake na kutoa masharti kwa kipindi ambacho kitaelezwa kwenye kibali.

Alisema kuchukua maji zaidi ya yale yaliyoidhinishwa katika kibali na kwa kuzingatia sheria za matumizi ya maji ni kosa kisheria na anakamatwa anaweza kulipa faini au kufungwa.

Alisema endapo kutokana na ukame au majanga ya asili kiasi cha maji kwenye chanzo chochote hakitoshi au hakitatosha kukidhi mahitaji, Bodi ya Maji ya Bonde inaweza kusitisha kwa muda au kurekebisha vibali vyote au chochote kwenye chanzo hicho kwa kadri itakavyoona inafaa.

Mmoja wa wananchi wa eneo hilo aliyekutwa akifukua mchanga katika bonde la mto Ruaha ili apate maji kwa matumizi yake, Rajabu Ismail alisema; “mto huu hauna historia ya kukauka kama ilivyotokea katika kipindi hiki.”

Alisema kilio cha wananchi kuhusu maji katika eneo hilo, kilipelekea wabaini hujuma inayofanywa na kampuni hiyo kwa maslai yake binafsi.

Alisema mbali na wakulima kuathiriwa na hatua hiyo, viumbe hai wakiwemo samaki na mamba wanaendelea kufa kwasababu ya kukosa maji.

Naye Mathias Khatibu wa kijiji cha Imalosongwe alisema; “mahusiano kati ya wananchi na mwekezaji huyo sio mazuri hali inayowapa hofu baadhi ya wananchi hususani wafugaji ambao kwa kukosa maji katika maeneo yao, wanalazimika kwenda katika maeneo ya mwekezaji.”

Diwani wa kata hiyo, Chuki Jeremia alisema anazo taarifa za wafugaji kwenda kandokando ya maeneo ya kampuni hiyo na kuchunga mifugo yao.

“Kumekuwepo na taarifa za wananchi kukamatwa na wakati mwingine kusababisha maafa jambo linaloleta haja ya kutafuta namna ya kuboresha mahusiano na mwekezaji huyo,” alisema.

Hadi tunakwenda mitamboni, mmoja wa wakurugenzi wa kampuni hiyo, Haroon Mulla ambaye hakuweza kupatikana kuzungumzia tuhuma hiyo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment