Friday, 16 December 2016

MWANZISHILI WA JAMII FORUMS AFIKISHWA MAHAKAMANI, AKOSA MDHAMINI


MWANZILISHI wa Mtandao wa JamiiForums aliyekamatwa na Polisi kuanzia juzi Maxence Melo, leo amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisitu Jijini Dar es Salaam na kusomewa mashtaka matatu.

Melo amefikishwa mahakamani baada ya sitofahamu iliyokuwa imetanda kuhusu kosa lililosababisha kukamatwa kwake na kabla ya tukio hilo Polisi walifanya upekuzi ofisini na nyumbani kwake.

Baada ya kupanda kizimbani, Melo amesomewa mashtaka matatu yanayomkabili likiwemo la kumiliki na kuendesha tovuti ambayo haijasajiliwa hapa nchini Tanzania (JamiiForums).

Mashtaka mengine ni kuzuia na kuharibu taarifa ambazo Jeshi la Polisi wamekuwa wakizitaka kwa ajili ya uchanguzi chini ya kifungu cha 22 cha Sheria ya Makosa ya Mitandao na kushindwa kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi  na kuharibu uchunguzi chini ya kifungu cha namba 22 cha Sheria ya Makosa ya Mitandao.

Kwa mujibu wa taarifa zilizokuwa zimetolewa na tovuti ya JamiiForums jana, walisema kuwa ‘server’ ya tovuti yao haipo nchini Tanzania wala barani Afrika lakini hawakutaja ni nchi gani ilipo.

Melo amepelekwa rumande Keko hadi Jumatatu Disemba 19 mwaka huu baada ya kukosa mdhamini katika shtaka la tatu la kumiliki na kuendesha tovuti ambayo haijasajiliwa nchini.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment