Sunday, 18 December 2016

MAWAKALA WA PEMBEJEO IRINGA WAITUHUMU TFC


MAWAKALA wa pembejeo za kilimo wa wilayani Iringa wameingia katika vita ya maneno na Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) wakihituhumu kuwa na upendeleo katika utuezi wa mawakala watakaofanya nao kazi katika msimu huu wa kilimo.

Kati ya mawakala 33 walioomba kuifanya kazi hiyo katika msimu huo wilayani humo, ni mawakala 11 tu walioteuliwa na TFC kushirikiana nao kuifanya kazi hiyo.

Serikali iliamua kuitumia TFC kusambaza pembejeo za ruzuku kwa kile kilichoelezwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Pembejeo wa Wizara ya Kilimo, Shanel Nyoni kwamba hatua hiyo inalenga kuongeza udhibiti na kumaliza udanganyifu.

Ili kufanikisha jukumu hilo, TFC ilipewa pia jukumu la kuteua mawakala itakaosaidiana nao kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi.

Wakizungumza na wanahabari jana, mawakala zaidi ya 20 waliituhumu TFC wakisema utuezi wa mawakala hao umejaa hila, una harufu ya rushwa na unalenga kuwaweka katika mazingira magumu ya biashara hiyo wale waliotemwa.

Mmoja wa mawakala hao, Aurelia Kaundama alisema kwa kupitia TFC serikali imewatema kuifanya kazi hiyo msimu huu pamoja na kwamba wanaidai mamilioni ya fedha za msimu wa kilimo uliopita.

 “Binafsi naidai serikali zaidi ya Sh Milioni 45 baada ya kusambaza pembejeo hizo katika kata ya Kalenga na Uwanda msimu wa kilimo uliopita, inashangaza natemwa katika mazingira haya bila kulipwa deni langu” alisema.

Naye Ferdinand Mahalila anayeidai serikali Sh Milioni 32 baada ya kusambaza pembejeo hizo msimu uliopita alisema; “Tuna wasiwasi mkubwa wa namna TFC ilivyopata mawakala wa kufanya nao kazi katika msimu wake huu wa kwanza.”

Kwa upande wake, Melicho Magoyo alisema serikali kwa kupitia TFC inataka kuwaadhiri kwani inajua kwamba wanaidai, na wao wanadaiwa lakini imewanyima kazi hiyo mwaka huu na kutoa kwa baadhi ya mawakala wasiojulikana katika maeneo yao.

Caristo Gwido alisema lingekuwa jambo la busara kama wangelipwa kwanza madeni yao kabla ya kuondolewa kuifanya kazi hiyo.

Afisa wa TFC Mkoani Iringa, Judica Mollel alikwepa tuhuma hiyo akisema uteuzi wa mawakala unafanywa na “TFC makao makuu, sio mimi kama wanavyofikiri.”

Alisema katika kuteua mawakala hao, yapo mambo ya msingi ambayo TFC inayazingatia ikiwa ni pamoja na uaminifu na ambao wamefanya kazi na TFC kwa miaka mitatu mfululizo na wala hakuna upendeleo, hila na rushwa katika hayo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Pembejeo ya Wilaya ya Iringa ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela alisema  baada ya mfumo wa kupata mawakala kubadilika kazi hiyo hafanywi tena na kamati kama yake kama ilivyokuwa mwanzo na badala yake inafanywa na TFC.

“Tulipenda mawakala wetu wengi wapate kazi hii, lakini TFC wana vigezo vyao na sisi hatuwezi kuwaingilia japokuwa tunaweza kuwashauri,” alisema.

Katika kuwapoza mawakala waliotemwa, Mkuu wa Wilaya alisema ofisi yake na ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa inaendelea kufuatilia madeni ambayo mawakala hao wanaidai serikali ili waweze kulipwa.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment