Thursday, 1 December 2016

KITISI FC WACHUKUA KOMBE LA SPANEST, WAONDOKA NA ZAWADI LUKUKI
KLABU ya Kitisi imeshinda Kombe la SPANEST linalodhaminiwa na Mradi wa Kuboresha Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania baada ya kuwashinda Kinyika FC kwa mikwaju ya penati 4-2.

Dakika 90 za mchezo huo uliopigwa katika uwanja maarufu wa Kimande Pawaga, Iringa Vijijini ulishuhudia wababe hao waliovuka vihunzi dhidi ya timu nyingine 22 zinazozunguka hifadhi ya Taifa ya Ruaha, wakitoka sara ya 1-1 mbele ya mashabiki waliokadiriwa kuwa zaidi ya 3,000.

Kwa ushindi huo, Kitisi FC iliondoka na kombe, medali za dhahabu, seti moja ya jezi, cheti na Sh Milioni moja taslimu huku wakiahidiwa kutembelea hifadhi ya Ruaha.

Watakapofanya ziara katika hifadhi hiyo, Kitisi FC watapata pia fursa ya kumenyana na timu kali ya waandishi wa habari wa mkoa wa Iringa inayoundwa na wachezaji mahiri 20.

Pamoja na kwamba Kinyika FC waliokuwa na matumaini makubwa ya kutwaa kombe hilo baada ya kuongoza kwa muda mrefu katika dakika 90 za mchezo, kulizwa kwa mikwaju ya penati, wameondoka na medali za shaba, cheti, mipira miwili na Sh 700,000 taslimu.

Nafasi ya tatu ya ligi hiyo ilikwenda kwa Itunundu FC, waliofanikiwa kumlaza kwa mabao 3-2 Mapogolo FC ambao pia walipata zawadi mbalimbali kutoka kwa waandaji wa mashindano hayo ya kila mwaka yanayolenga kuwaokoa Tembo dhidi ya majangili.

Akikabidhi zawadi kwa washindi, Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela aliahidi kusaidia kuyatafutiwa wadhamini zaidi kwa kuwa yana mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya majangili.

Mratibu wa SPANEST inayoratibu mashindano hayo, Godwell Ole Meing’ataki alisema fainali ya ligi hiyo inalenga kuoa Tembo kwa kupitia kauli mbiu yake ya “Piga Vita Ujangili, Piga Mpira Okoa Tembo.” 


Meing’ataki alisema wazo la kuunganisha vijana katika vita ya ujangili linaonekana kuwa njia muafaka ya kutokomeza ujangili kutokana na ukweli kwamba vijana ndiyo walengwa wakubwa katika kushawishika kuingia kwenye maeneo yaliyohifadhiwa na kufanya ujangili.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment