Saturday, 31 December 2016

KASESELA AKIPIGA JEKI KIKUNDI CHA WANAHABARI WAOSHA MAGARI

MKUU wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela ametoa msaada wa mashine moja ya kuoshea magari kwa wanahabari 10 wanaounda kikundi cha Wanahabari Waosha Magari Iringa (WWM).

Mashine hiyo yenye thamani ya Sh Milioni Moja ilikabidhiwa jana kwa Mwenyekiti wa kikundi hicho, Frank Leonard ambaye pia ni Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa (IPC).

Mbali na Leonard, wengine wanaounda kikundi hicho ni Irine Mwakalinga, Tukuswiga Mwaisumbe, Ester Malibiche, Zuhura Zukheri, Peter Naminga, Godfrey Nyang’oro, Denis Mlowe, Clement Sanga na Agustino Kihombo.

Pamoja na mashine hiyo, Kasesela alitoa mchango wa Sh 100,000 kwa kikundi hicho kinachohitaji mashine ya kuvuta vumbi na kusafisha ndani ya gari, tenki za kuhifadhi maji na vifaa vingine vya usafi wa magari.

Akikabidhi msaada huo, alisema; “nawaomba wadau wenngine mjitokeze kukiinua kikundi hiki ili kiwe mfano kati ya vikundi vya wanahabari wajasiriamali.

Kasesela alisema nia yake ni kuona wanahabari pamoja na kupata kipato kwa kazi wanazofanya lakini wanakuwa na shughuli zingine zitakazoinua kipato na kuboresha maisha yao.

Alisema kama wanavyofanya kazi ya kuhamasisha maendeleo ya watu wengine, wanahabari nao hawatakiwi kusahau kwamba wao pia ni sehemu ya maendeleo hayo na wanapaswa kushiriki kwa vitendo.

Alisema amefanya kazi na wanahabari wengi nchini na anaikubali kazi yao inayosaidia kuwainua watu wengi kisiasa, kiuchumi na kijamii, lakini anashangazwa na jinsi wengi wao wanavyoishi maisha yasiyoridhisha.

“Waandishi wa habari wamekuwa ngazi ya viongozi na wanasiasa wengi, lakini wamekuwa wakisahauliwa mara baada ya viongozi na wanasiasa hao kupata mafanikio wanayoyataka,” alisema.

Aliwaomba viongozi na wanasiasa hao kuwarudia wanahabari waliowasaidia kufanikisha mambo yao na kuwasaidia si kwa kuwapa posho bali kwa kuwawezesha ili wawe na shughuli za kijasiriamali zitakazoinua maisha yao.

“Nimeanza na kikundi hiki, nataka kiwe mfano kwa wahanabari wengine nchini, kioneshe kwa vitendo kuufunga mwaka 2016 na kuingia mwaka 2017 kikiwa na kauli mbili ya umasikini sasa mwisho,” alisema.

Alisema kikiwa na malengo na kikawa na nidhamu ya matumizi ya fedha watakazopata, kikundi hicho kitaleta tija katika kipindi kifupi kijacho.


Wakati huo huo, Kasesela amewatakia wakazi wa wilaya yake na watanzania kwa ujumla heri ya mwaka mpya huku akiwataka wauanza mwaka 2017 wakianzisha shughuli za kijasiriamali zitakazowaongezea kipato.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment