Sunday, 4 December 2016

KAMPUNI YA UTALII YA CHABO AFRICA YAPATA TUZO, YAISHAURI SERIKALI

KAMPUNI ya Chabo Afrika inayojishughulisha na usafirishaji watalii imeiomba serikali kuzipunguzia kodi kampuni zinazotoa huduma hiyo kusini mwa Tanzania ili kuzisaidia kuboresha huduma zake na utalii katika mikoa hiyo.

Mmoja wa wakurugenzi wa kampuni hiyo iliyopata ushindi wa jumla katika maonesho ya Karibu Kusini na Siku ya Utalii Duniani iliyofanyika kitaifa mjini Iringa wiki iliyopita, Ernest Lugalla alisema:

“Tunalipa Dola 2,000 sawa na zaidi ya Sh Milioni 4 kwa mwaka, kuendesha kampuni ya Utalii pamoja na kwamba biashara ya utalii kusini ni ndogo sana ikilinganishwa na kaskazini.

Lugalla alisema udogo wa biashara ya utalii katika ukanda huo, umewafanya watu wengi wenye kampuni za utalii kuogopa kusogea katika mikoa hiyo na badala yake kuendelea kujikita katika mikoa ya kaskazini kunakodaiwa kuwa na mazingira mazuri ya biashara hiyo.

“Kama kweli serikali ina dhamira ya kuutangaza utalii na inataka kuinua shughuli za utalii katika mikoa hii kuna haja ikatuangalia kwa jicho la kutuhamasisha,” alisema.

Mbali na kuwapunguzia kodi na gharama zingine za uendeshaji, alisema serikali ina wajibu wa kuboresha miundombinu na kuwahamasisha wadau wengine wakiwemo wa huduma za hoteli kujenga hoteli nzuri na zenye hadhi ya kitaifa na kimataifa.

Akitoa mfano; alisema barabara za kwenda hifadhi ya Taifa ya Ruha, Udzungwa na Kitulo; na huduma katika hoteli nyingi mara nyingi zimekuwa katika hali mbaya inayolalamikiwa na watalii wanaotembelea vivutio vilivyoko katika mikoa hiyo.

Mmoja wa watembaza watalii kutoka katika kampuni hiyo, Frank Ndosi alisema; “Changamoto hizo zinafunika uzuri wa vivutio vilivyoko katika mikoa ya kusini na akaomba serikali ichukue hatua za haraka kuzishughulikia.”

Akitoa mfano wa uzuri wa vivutio hivyo, Ndosi alisema katika hifadhi ya Ruaha ambayo ni kubwa kuliko zote nchini, Simba 10 wanaweza kushuhudiwa kwa mara moja na watu waliopo katika gari moja wakati kule kaskazini ni kawaida magari zaidi ya 10 kurundikana mahali palipo na Simba mmoja.

Akijibu maombi ya kampuni hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alisema biashara ya utalii inalipa na haitakiwi kufanywa kama biashara ya Taxi bubu.

“Ipo mifano dhahiri kabisa, zipo kampuni zinatengeneza zaidi ya Sh Milioni 100 kwa safari moja ya kutembeza watalii 10 tu katika hifadhi zetu, kwa mazingira hayo mnashindwaje kulipa Sh Milioni 4,” alisema.


Kuhusu miundombinu ya barabara na usafiri wa anga , Profesa Maghembe alisema serikali inaendelea kuziboresha huduma hizo na akawataka wafanyabiashara wenye uwezo kuwekeza katika mikoa ya kusini kwa kujenga hoteli zenye hadhi kwa watalii wote.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment