Monday, 26 December 2016

DK MWANDULAMI ATUMIA MILIONI 65 KUSAMBAZA MAJI KIJIJINI KWAKE
MGANGA maarufu wa tiba asili wa wilayani Njombe mkoani Njombe, Dk Antony Mwandulami ametumia zaidi ya Sh Milioni 65 kushughulikia changamoto ya upatikanaji na usambazaji wa maji iliyokuwa ikikikabiri kijiji chake cha Itunduma, wilayani humo.

Akizungumzia na wanahabari waliotembelea kijijini hapo hivikaribuni, Mwenyekiti wa kijiji hicho,  Medson Nyagawa alisema kabla ya kushughulikia tatizo hilo wananchi wa kijiji hicho walikuwa wanatembea zaidi ya kilomita tano kutafuta maji.

Kwa kupitia fedha hizo, Nyagawa alisema, Dk Mwandulami alihifadhi na kuanza kukilinda chanzo cha maji cha Nyhengeza, alichimba bwawa katika chanzo hicho, alipeleka umeme na pampu ya kusukuma maji na akajenga tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita 32,000 za maji.

“Pamoja na kujenga tenki hilo akatengeneza mtandao wa kusambaza maji kwa wananchi na kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji,” alisema huku akimshukuru mganga huyo kwa mchango huo kwa jamii inayomzunguka.

Akizungumzia sababu za kujitolea kuikabili changamoto hiyo, Dk Mwandulami alisema; “kama mkazi wa kijiji hiki niliguswa sana na tatizo la ukosefu wa maji na ndipo nikaamua kikifufua chanzo hicho kilichopo mita 200 kutoka brabara kuu ya Njombe Makambako.”

Alisema chanzo hicho chenye chemichemi nyingi kilikauka kutokana na kukithiri kwa shughuli za kilimo, ufugaji na ukataji wa miti.

“Nilianza kwa kutumia zaidi ya Sh Milioni 18 kukirudisha chanzo hicho katika hali yake ya kawaida na kwa kushirikiana na serikali ya kijiji tukakihifadhi na kukilinda hadi kikaleta mafanikio yote hayo,” alisema.

Dk Mwandulami alisema baada ya kuanza kutiririsha maji alilazimika kujenga bwawa pembeni yake, akapandikiza samaki wa aina mbalimbali na kujenga njia za maji za kisasa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.

“Mbali na bwawa hilo kuwezesha usambazaji wa maji majumbani na mashambani lakini limetoa ajira inayowaongezea kipato vijana wanaojishughulisha na uvuvi,” Dk Mwandulami alisema huku akiahidi kuendelea kuchangia maendeleo ya kijiji chake hicho.

Alivitaka vijiji vyenye changamoto ya maji viende kijijini hapo vikajifunze namna bora na rahisi ya kuhifadhi na kulinda vyanzo vya maji kwa manufaa yao na ya vizazi vijavyo akisema maji ni uhai na ni maendeleo.

Mmoja wa vijana anayefanya shughuli ya uvuzi katika bwawa hilo, Samsoni Mwinami alimshukuru Dk Mwandulami akisema mchango wake huo, umemuhakikishia kupata wastani wa Sh 10,000 kila siku kutoka katika shughuli yake yake ya uvuvi katika bwawa hilo.

Naye Doris Mtelele alisema; “kwa pamoja miradi hiyo imetuondolea hofu ya kubakwa wakati tukitembea umbali mrefu kutafuta maji.”


Mwenyekiti wa kitongoji cha Ibumilahenga yalipo makazi ya mganga huyo, Koresi Mwalongo alisema pamoja na mradi huo, kijiji hicho kinapata maji mengine kupitia mradi wa Tove na hivyo kumaliza kabisa tatizo la maji kwa matumizi ya wananchi na mashambani.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment