Tuesday, 13 December 2016

CWT MKOA WA IRINGA WAPOKEA MSAADA WA MIPIRA 229
CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) mkoa wa Iringa kimepokea mipira 229 CWT Taifa na kuigawa jana kwa viongozi wa CWT ngazi ya wilaya na mkoa huo.

Mipira hiyo ambayo hata hivyo thamani yake haikuweza kujilikana mara moja ni kwa ajili ya mpira wa miguu, kikapu na wavu.

Katibu wa CWT Mkoa wa Iringa Francis Msisi alisema; “mipira hii ni sehemu ya mipira iliyotolewa na CWT nchi nzima kwa ajili ya kuwawezesha walimu, hasa vijana kushiriki katika michezo.”

Wakati CWT mkoa wa Iringa wanapata mipira tisa, Msisi alisema kila chama mkoani humo kitapata mipira 55.

“Tuna wilaya ya Mufindi, Kilolo, Iringa Vijijini na Manispaa ya Iringa; kila wilaya inapata mipira 55 ambayo kati yake 50 ni kwa ajili ya mpira wa miguu, mpira wa wavu mwili na mpira wa kikapu mitatu,” alisema.

Akikabidhi mipira hiyo kwa viongozi wa CWT wa wilaya hizo, Mwenyekiti wa CWT Mkoa wa Iringa Stanslaus Mhongole alisema; “walimu tumeamua kufurahia Tanzania yetu baada ya miaka 55 ya Uhuru kwa kushiriki michezo.”

Alisema CWT inahamasisha michezo kwa walimu wake baada ya kuanzisha kitengo cha vijana katika chama hicho.

“Asilimia 85 ya walimu ni vijana, tusipowapa fursa ya kukutana na kufurahi kwa pamoja ni hatari, tumeamua wakutane kupitia michezo,” alisema.

Alisema kwa kupitia mpango huo, wataunda timu za walimu wa ngazi ya kata na baadaye wilaya huku mipango yao ya baadae ni kuwa na timu zitakazoshiriki michezo hiyo katika ligi mbalimbali.

Mwakilishi wa Vijana wa CWT Mkoa wa Iringa, James Asagwile alipongeza hatua hiyo akisema itasaidia kuimarisha chama hicho na kukuza mahusiano yao miongoni mwao

Reactions:

0 comments:

Post a Comment