Wednesday, 14 December 2016

CWT IRINGA YAMPIGIA MAGOTI MAGUFULI


CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT) Mkoa wa Iringa kimempigia magoti Rais Dk John Magufuli kikimuomba azungumze lolote kuhusu madai ya walimu wakati wakijiandaa kuingia mwaka mpya.

Akizungumza na wanahabari jana, Mwenyekiti wa CWT Mkoa wa Iringa, Stanslaus Mhongole alisema katika kipindi ambacho baadhi ya watanzania wanalalamikia ukata, kwa upande wao ni kama madai yao ya msingi yamesimama kushughulikiwa.

“Tunamuomba Rais awape walimu furaha, aondoe ukimya juu yetu, natamani kabla mwaka haujaisha asema chochote kuhusu madai yetu maana tumepiga kelele kwa miaka mingi” alisema.

Mbali na madeni aliyosema yanaendelea kushughulikiwa na serikali, Mhongole aliyataja madai yao mengine ya msingi kuwa ni pamoja na posho ya kufundishia na upandaji wa madaraja.

Alisema posho ni kilio chao cha muda mrefu ni upandaji wa madaraja ni jambo linalomuondoa mwalimu kutoka katika ngazi moja ya mshahara kwenda ngazi nyingine.

Alisema kwa miaka mingi walimu wamekuwa wanyonge katika Taifa na akamuomba Rais Magufuli ambaye ni kiongozi aliyedhamiria kuwasaidia wanyonge wan chi hii, kutupia jicho la haraka kwa walimu.

“Kama madaktari, wanajeshi na watumishi wengine wanapata posho, kwanini walimu ambao kazi yao kubwa ni kutengeneza akili za watu wakiwemo viongozi na watalaamu wa nchi hii, hawatazamwi ipasavyo?” alisema.

Aliipongeza serikali ya Dk Magufuli kwa kuanza kutoa posho kwa wakuu wa shule na waratibu wa elimu lakini akasema walimu wa shika kazi wanapaswa kutazamwa kwa jicho hilo hilo kutokana na ugumu na unyeti wa kazi yao.

“Na niipongeze pia serikali yake kwa kuandika historia nyingine katika maendeleo ya sekta hiyo. Kwa mara ya kwanza mwaka huu, walimu waliosimamia mitihadi ya darasa la nne walipata posho, haijawahi kutokea,” alisema.


Pamoja na jitihada hizo, Mhongole aliuliza ni lini Dk Magufuli atakutana na CWT ili waweze kumueleza changamoto zao kwa kina.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment