Thursday, 29 December 2016

BAADA YA KUFUNGWA KOLA, HAKUNA TEMBO ALIYEUAWA RUAHA


HIFADHI ya Taifa ya Ruaha imesema haina taarifa ya Tembo yoyote kuuawa katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita baada ya wanyapori hao kufungwa kifaa maalumu (kola) kinachofuatilia mienendo yao ya ndani na nje ya mfumo wa Ikolojia ya Ruaha.

Akizungumza na wahabahari hivikaribuni, Kaimu Mhifadhi Mkuu wa hifadhi hiyo, Moronda Moronda aliupongeza utaratibu huo akisema umesaidia kuimarisha usalama wa wanyama hao wanaowindwa na majangiri usiku na mchana kwa kuwaongezea ulinzi popote walipo.

“Lakini pia mfumo huu unaotumia teknolojia ya kisasa ya mawasiliano ya setilaiti ya utambuzi wa jiografia ya maeneo (GPS) na kompyuta, umesaidia pia kupunguza migogoro kati ya vijiji na wanyama hao,” alisema.

Akifafanua alisema mfumo huo unawezesha kujua mahali popote yalipo makundi ya Tembo, kuwadhibiti wasiendelee kufanya madhara katika vijiji jirani na hifadhi hiyo na kuwarudisha hifadhini.

Shughuli ya ufungaji Kola kwa Tembo hao ulifanywa Novemba mwaka jana na Taasisi ya World Elephant Centre (WEC) kwa kupitia Mradi wa Kuboresha Mtandao wa Maeneo ya Hifadhi Kusini mwa Tanzania (SPANEST) unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

Mtafiti Mwandamizi wa WEC, Dk Alfred Kikoti alisema kwa kupitia teknolojia hiyo, mienendo ya wanyama hayo inaripotiwa  kwenye setilaiti na kurushwa moja kwa moja katika chumba maalumu cha ulinzi.

“Kwahiyo teknolojia hii inatuwezesha kujua mwenendo wa tembo ndani na nje ya hifadhi; kujua walipo, wanapopita, kasi yao ya kutembea, sehemu wanazojificha, wanazokunywa maji, wanazopumzika na maeneo wanayokaa kwa muda mrefu,” alisema.

Pamoja na hayo alisema tekenolojia hiyo inawezesha kujua kama wamekufa, wamejeruhiwa, wamehama hifadhi moja hadi nyingie na taarifa nyingine nyingi hivyo kuongeza urahisi kwa askari wa wanyamapori kufuatilia usalama wao. 

Dk Kikoti alisema kwa kuzingatia kwamba Tembo wana kawaida ya kutembea katika makundi makubwa, Kola hizo zenye uwezo wa kufanya kazi kwa miaka mitatu bila kubadili betri zake zimefungwa kwa Tembo 30 wanaoongoza makundi 30. 

Alisema baada ya kukamilika kwa zoezi hilo lililogharimu Dola 15,000 (Sawa na Sh Milioni 30) kwa Tembo mmoja, askari wa doria wanafanya kazi hiyo kwa kuongozwa na taarifa zinazotolewa na kola tofauti na hapo awali ilipokuwa ikifanywa kwa kukisia tu.

“Zoezi la ufungaji kola kwa tembo mmoja huchukua wastani wa dakika 30, likihusisha matumizi ya helkopta kwa ajili ya kubaini yalipo makundi ya Tembo na uchomaji wa sindano ya usingizi kwa Tembo anayefungwa Kola, ufungaji wa Kola na uchomaji wa sindano ya kumzindua,” alisema. 

Akizungumzia mafanikio ya mpango huo, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Allan Kijazi alisema eneo la mfumo wa ikolojia ya Ruaha ni kubwa na lina tembo wengi kuliko eneo jingine Tanzania hivyo haina budi kuangaliwa kwa ukaribu zaidi.

“Tunafurahi kwamba Kola hizo zimeunganishwa na mifumo ya mawasiliano na kuliwezesha shirika kufanya kazi ya ulinzi kwa ufanisi zaidi kwa kuhakikisha kila wanapokuwepo wanyama hao, askari wanakuwepo pia,” alisema.


Naye Mratibu wa SPANEST, Godwel Ole Meing’ataki alisema zoezi la ufungaji wa kola kwa tembo ni moja ya shughuli ya mradi huo katika harakati za kuwalinda tembo na kupambana na ujangili.

Alisema kwa kupitia kifaa hicho askari wa wanyamapori watakabiliana kirahisi na majangili wa meno ya tembo katika azma ile ile ya kunusuru kiumbe hicho kinacholiingizia Taifa fedha nyingi za kigeni.

Pamoja na Tembo hao kufungwa kifaa hicho, Meing’ataki alisema wadau wa uhifadhi hawana budi kuendelea na mikakati mingine ya kukabiliana na ujangili ili kwa pamoja mipango hiyo imalize kabisa tatizo hilo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment