Sunday, 18 December 2016

AOMBA ASAIDIWE KULIPWA DENI LAKE LA MILIONI 16


MFANYAKAZI wa Huruma Babtist Confrence Centre ya mjini Iringa, Aidan Kalenge ameziomba mamlaka zinazohusika kumsaidia kupata malipo yake ya zaidi ya Sh Milioni 16 anazoidai taasisi hiyo.

Akizungumza na Habarileo jana, Kalenge alisema fedha hizo ni za mshahara wake wa toka mwaka 2003 hadi sasa alipofukuzwa kazi kwa madai ya wizi yaliyoshindwa kuthibitishwa.

“Walisitisha kunilipa mshahara Machi 2003, lakini nilirudi kazini Novemba 2005 baada ya Waziri wa Kazi kutengua uamuzi wa taasisi hiyo dhidi yangu kwa kuwa haukufuata taratibu,” alisema.

Kwa kupitia barua ya Novemba  15, 2005 iliyosainiwa na Waziri wa Kazi wa wakati huo, Profesa Juma Kapuya(nakala yake tunayo), waziri huyo alitengua maamuzi ya taasisi hiyo ya kumfukuza kazi Kalenge kwa mujibu wa kifungu cha 26 (2) cha Sheria ya Usalama Kazini ya 1964, sura ya 574.

“Kwa kupitia kifungu hicho natengua uamuzi wa Baraza la Usuluhishi kuwa mfanyakazi aachishwe kazi na badala yake naamua arudishwe kazini na kulipwa haki zake zote tangu kufukuzwa kwake kwasababu tuhuma dhidi yake hazikuthibitika,” inasomeka barua hiyo ya Kapuya.

Pamoja na agizo hilo, Kalenge alisema uongozi wa taasisi hiyo haukumpokea na haukumruhusu kuendelea na kazi ya muhudumu wa mapokezi aliyokuwa hakiifanya.

“Naomba Rais na Waziri Mkuu aingilie kati, mimi ni mwananchi masikini, nimefuatilia haki yangu toka wakati huo hadi sasa bila mafanikio, na kwa hesabu za haraka nadai zaidi ya Sh Milioni 16,” alisema.

Akikana madai hayo, mmoja wa viongozi wa Huruma Babtist Conference Centre, Daimoni Mwaipopo alisema hawezi kuyazungumzia madai ya Kalenge kwa kina kwasababu taasisi iliyokuwa imemuajiri kwasasa haipo.

“Huruma Babtist Conference Centre iliyokuwa inatoa huduma za hoteli na kumbi za mikutano mjini Iringa kwasasa haipo,” alisema bila kusema lini taasisi hiyo ilifutwa.

Alisema baada ya taasisi hiyo kufutwa, mejengo yake yalilithiwa na shule ya sekondari ya wasichana ya Spring Valley ambayo yeye ni Meneja wake.


“Na hakuna mahusiano yoyote kati ya Huruma Babtist Conference Centre na sekondari ya Spring Valley kwasababu hivyo ni vitu viwili tofauti,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment