Saturday, 10 December 2016

ACCESSBANK YAZINDUA TAWI MJINI IRINGA KWA KISHINDO

ACCESSBANK imezindua tawi lake jipya mjini Iringa huku ikitoa mikopo 515 yenye thamani ya zaidi ya Sh Milioni 982 kwa baadhi ya wakulima wa mkoa huo, itakayotumika kuongeza tija katika sekta ya kilimo.

Uzinduzi wa tawi hilo, linalokuwa tawi la 13 la benki hiyo nchini, ulifanywa na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi na wadau mbalimbali wa sekta ya fedha mkoani Iringa.

Mkuu wa maendeleo ya biashara wa benki hiyo, Andrea Ottina alisema ufunguzi wa tawi la benki hiyo mjini Iringa ni ushahidi wa dhamira yao ya dhati ya kutoa huduma bora kwa wateja wao nchini.

“Pamoja na kutoa huduma bora kwa wateja wetu, tunataka wapate huduma zetu kwa wakati pamoja na kuimarisha urahisi wa huduma za kibenki,” alisema.

Ottina alisema Iringa ni miongoni mwa mikoa inayokua kwa kasi nchini kutokana na upatikanaji wa vivutio vingi, uwekezaji na uzalishaji wa chakula cha mazao ya biashara.

Kwa kupitia tawi hilo, alisema wakulima na wajasiriamali wa mkoa wa Iringa watafaidika sana na huduma za benki hiyo.

Alisema benki hiyo itaendelea kupanua huduma zake ili kufikia sehemu kubwa ya wateja nchini kote, pamoja na kuanzisha bidhaa na njia mpya za upataji huduma.

“Njia hizo ni kama vile huduma za kibenki kupitia simu ya mkononi na wakala wa kibenki ambao wamelengwa zaidi katika maeneo ya vijijini na mijini pia,” alisema.

Akizundua tawi hilo, Masenza aliipongeza benki hiyo kwa kuongeza urahisi wa upatikanaji wa huduma bora za kifedha katika mkoa wa Iringa.

“Natoa wito kwa wakulima na wajasiriamali, wafanyabishara wakubwa na wadogo kuchukua faida ya huduma zinazotolewa na benki hii kama fursa ya kuendeleza shughuli zenu za kilimo na biashara,” alisema.

Alisema sekta ya benki ni muhimu katika maendeleo ya Taifa kwani ndiyo inayowezesha uwekezaji unaoweza kuleta mabadiliko kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

“Matarajio yangu ni kuona mnaendelea kutoa huduma itakayokuwa na mfuto, msiwe sehemu ya wale wanaonyanyasa wananchi katika utoaji wa huduma za kifedha,” alisema.

Awali Meneja wa tawi la AccessBank mkoani Iringa, Frederick Masungwa alisema benki hiyo ilianza kutoa huduma zake za kifedha mkoani hapa, Julai mwaka huu na hadi Novemba mwaka huu ilikuwa na wateja zaidi ya 3,000.

Masungwa alisema benki hiyo inatoa huduma za akaunti mbalimbali ikiwemo ya akiba, kikundi, hundi, amana, mikakati, wanafunzi, wafanyabishara wakubwa; na pia inatoa huduma za kutuma fedha ndani na nje ya nchi na huduma ya ATM kupitia Umoja Switch.

Alisema tangu waanze kutoa huduma hizo,katika kipindi cha miezi sita iliyopita mkoani Iringa wamekwishapata wateja zaidi ya 3,000.


AccessBank ni taasisi ya kifedha inayolenga kutoa huduma za kibenki kwa wajasiriamali wadogo na wa kati kupitia wanahisa wake wa kimataifa ambao ni AccessHolding, International Finance Corporation, African Development Bank na MicroVest.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment