Tuesday, 29 November 2016

VYUO VIKUU VINAVYOTAKIWA KUFUTWA VYAKINGIWA KIFUACHUO Kikuu cha Katoliki Ruaha (RUCU) cha mjini Iringa kimevikingia kifua vyuo vikuu vinavyotakiwa kufutwa kwa madai ya kukosa sifa, kikiiomba serikali isichukue uamuzi huo na badala yake ivishauri na kuvisaidia kufikia viwango vinavyotakiwa.

Wakiongea kabla na wakati wa mahafali ya tisa ya chuo hicho yaliyofanyika chuo hapo juzi, viongozi wa chuo hicho walikiri kuwepo kwa vyuo visivyo na ubora lakini wakakumbusha kwamba vyote vilifanyiwa tathmini ya ubora unaotakiwa kabla ya kusajiliwa.

“Kama kuna tatizo la ubora sasa ni wajibu wa serikali kuvishauri na kuvisaidia vifikie hatua ya inayotakiwa kuliko kuvifunga,” alisema Naibu wa Makamu Mkuu wa RUCU, Profesa Gaudance Mpangala.

Profesa Mpangala alitaja athari nyingi ya kufuta vyuo hivyo ikiwemo ile aliyosema itaporomosha zaidi udahili wa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini tofauti na nchi nyingine za Afrika Mashariki.

“Pamoja na kuwa na wanafunzi wengi wenye sifa za kujiunga na vyuo vikuu, kwa takwimu za sasa Tanzania ni ya mwisho kwa nchi za Afrika Mashariki zikiwemo nchi za Burundi na Rwanda kwa udahili wa wanafunzi wa vyuo vikuu,” alisema.  

Makamu Mkuu wa RUCU, Dk Cephas Mgimwa alisema sekta binafsi na ya umma zinapaswa kushirikiana na kukumbushana wajibu wa kila mmoja ili kuboresha viwango vinavyotakiwa.

Dk Mgimwa alisema wanaamini tamko la serikali la kuvifuta vyuo vinavyodaiwa kukosa sifa linalenga kuwakumbusha wamiliki wake kuzingatia viwango vinavyotakiwa.

“Sio suala jema kuvifunga vyuo hivyo, lakini ni jambo jema kuhakikisha vinaboreshwa kama tunataka taaluma isiporomoke,” alisema.

Alisema mfumo wa elimu katika nchi ni lazima uwe imara na wa kudumu ukifanyiwa maboresho ya mara kwa mara kulingana na mabadiliko badala ya kufuta au kubadili kama ilivyotokea kwa zilizokuwa shule za sekondari za ufundi kama Ifunda na Dar Tech.

“Leo tungekuwa na shule hizo za ufundi zinazoendeshwa kwa kuzingatia mabadiliko ya teknolojia, kwa vyovyote vile nchi ingepiga hatua kubwa zaidi katika mapinduzi ya sayansi na teknolojia,” alisema.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Iringa (IUCo), Profesa Joshua Madumla, alisema vyuo vyote vilianzishwa kwa lengo la kuisaidia nchi na watu wake kupiga hatua kubwa ya kielimu.

Alisema katika mzingira ya kawaida ya uendeshaji wa vyuo hivyo ni lazima pawepo na changamoto zinazoweza kutafutiwa ufumbuzi wa pamoja ili malengo yaliyowekwa yafikiwe kwa maendeleo ya nchi kwa kuwa nchi inahitaji wasomi.

Alisema vyuo vipya vinachangamoto nyingi zaidi na akaitaja mojawapo kuwa ni uhaba wa walimu unaosababisha watumie wale wenye sifa za chini.

“Hali hii imefanya viwango vya ubora wa elimu nchini vilalamikiwe kwasababu mahali penye uhaba wa walimu ni lazima pawe na tatizo hilo ambalo hata hivyo linaweza kushughulikiwa,” alisema.

Akiwatunuku vyeti wahitimu zaidi ya 1500 wa astashahada, stashahada, shahada, shahada ya uzamili na shahada ya uzamivu katika fani mbalimbali, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi, Tekenolojia na Ufundi, Profesa Simon Msanjila alisema moja ya vipaumbele vya serikali ya awamu ya tano ni kuboresha sekta ya elimu.

“Asiyekidhi vigezo vya ubora serikali haitamvumilia. Wahusika ni lazima watekeleze maelekezo ya ubora wa elimu yanayotolewa,” alisema.

Alisema ni vizuri vyuo vikuu vikaanza kuangalia uwezekano wa kujikita katika fani fulani badala ya kuwa vyuo vya kila fani jambo linalochangia kuporomosha ubora.

“Vyuo vingi vinataka kuwa na kozi nyingi kwa mgongo wa kujitanua lakini nyuma ya pazia vinataka kudahili wanafunzi wengi ili vipate ada nyingi,” alisema.

Profesa Msanjila alikwenda mbali zaidi kwa kuvitaka vyuo vinavyofungua matawi yake kila mahali nchini, vijitafakari kwa kuzingatia mipango, uwezo wake na maelekezo ya serikali.

Aliitaka RUCU kuwa mfano huku Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela akikitaka chuo hicho kuwa kituo kikubwa nchini cha elimu ya mawasiliano na teknolojia.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment