Tuesday, 29 November 2016

UN WATOA ELIMU YA SDGs CHUO KIKUU CHA IRINGA

KAMPENI ya kuelimisha jamii kuhusu Malengo 17 ya Dunia ya Maendeleo Endelevu (SDGs) inayofanywa Umoja wa Mataifa (UN) imetua mkoani Iringa kwa kupitia jamii ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Iringa (IUCo), waliopewa elimu hiyo juzi.

Mratibu Mkazi wa Mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN) na Mwakilishi wa Shirika la Maendeleo (UNDP), Alvaro Rodriguez alisema katika kampeni hiyo kwamba kila mtu mwenye utashi ana wajibu wa kuyapigia debe malengo hayo.

Alisema malengo hayo ambayo pamoja na mambo mengine yanalenga kutokomeza umasikini, kuondoa njaa, usawa wa kijinsia na kuondoa utoafuti wa kipato yalipitishwa na nchi wanachama wa UN, Septemba mwaka jana  ili kuweka ustawi wa watu wote ifikapo mwaka 2030.

Rodriguez aliwasisitiza vijana hao kuwa mabalozi wa kusimamia utekelezaji wa malengo hayo nchini na kutumia maarifa yao kuyafikisha kwa vijana wengine na wananchi kwa ujumla.

Awali Mkuu wa Mawasiliano wa UN nchini, Hoyce Temu alisema Tanzania ni moja kati ya nchi 193 zilizoridhia malengo hayo, ikayathibitisha na kuyaingiza katika mipango yake ya maendeleo.

Ili kuchochea utekelezaji wake, Temu alisema kama ilivyo kwa nchi nyingine, UN nchini iliamua kuwa na program ya uelimishaji umma inayowalenga watanzania hususani vijana ikiamini kwa kupitia wao elimu hiyo itafika kwa wengine wengi.

Alisema kwa kupitia mijadala ya moja kwa moja UN inalenga kuwafikia kwa 30,000 wa vyuo vikuu na wengine 200,000 walioko nje ya taasisi hizo.

“Na kwa kutumia vyombo vya habari tunataka kuwafikia vijana milioni tano na watanzania milioni 15 kwa ujumla wake,” alisema.

Mwanafunzi wa IUCo Sabinus Paulo alisema yeye ni mmoja wa wanafunzi machampioni wanaoweza kusaidia dunia kuyatatekeleza malengo hayo, .

“Vijana tuna nguvu kubwa ya maamuzi na kufikiri, na tuna muda mwingi sana katika maisha tofauti na watu wengine, muda tunaoweza kuutumia kuisadia jamii kuyaelewa haya mambo” alisema.


Alisema anatumia ukurasa wake wa twitter na mitandao mingine ya kijamii kufanikisha na kuipa uwezo jamii inayomzunguka kwa kulifanyia kampeni lengo namba tano linalolenga kusimamia usawa wa kijinsia.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment