Wednesday, 16 November 2016

SPANEST CUP YAINGIA HATUA YA ROBO FAINALI
TIMU nane kati ya 24 zinazoshiriki ligi ya Kombe la SPANEST inayoendelea kupigwa katika viwanja mbalimbali vya soka wilayani Iringa zimefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali itakayoanza kuchezwa kesho.

Hatua hiyo itaziwezesha timu hizo Kitisi, Nyamahana , Makifu na Mapogoro za Tarafa ya Idodi na Luganga, Itunundu, Kinyika na Mbugani za Tarafa ya Pawaga kumenyana vikali kuwania kuingia fainali ya ligi hiyo.

Ligi hiyo inayochezwa kwa awamu ya pili toka ianzishwe miaka miwili iliyopita inaratibiwa na Mradi wa Kuboresha Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania (SPANEST).

Akikabidhi jezi na mipira itakayoziwesha timu hizo nane kushiriki vyema hatua hiyo, Mratibu wa SPANEST, Godwell Ole Meing’ataki alisema fainali ya ligi hiyo inayolenga kuoa Tembo kwa kupitia kauli mbiu yake ya “Piga Vita Ujangili, Piga Mpira Okoa Tembo” itapigwa Novemba 26, mwaka huu.

Alisema  robo fainali hiyo itapigwa kati ya Novemba 17 na 20, huku nusu fainali kwa timu nne zitakazoingia hatua hiyo ikitarajiwa kuchezwa Novemba 22.

Meing’ataki alisema zawadi kwa mshindi wa kwanza atakayepata kombe, medali, seti moja ya jezi, cheti na kutembelea hifadhi ya Ruaha imeongezeka kutoka Sh 300,000 hadi Sh Milioni moja.

Kwa upande wa mshindi wa pili atakayepata medali, cheti na mipira miwili imeongezeka kutoka Sh 200,000 hadi Sh 700,000 na ya mshindi wa tatu anayepata cheti na medali imeongezeka kutoka Sh 100,000 hadi Sh 500,000.

Meing’ataki alisema wazo la kuunganisha vijana katika vita ya ujangili linaonekana kuwa njia muafaka ya kutokomeza ujangili kutokana na ukweli kwamba vijana ndiyo walengwa wakubwa katika kushawishika kuingia kwenye maeneo yaliyohifadhiwa na kufanya ujangili. 

Reactions:

0 comments:

Post a Comment