Monday, 21 November 2016

MATUMIZI YA VYOO BORA IRINGA MANISPAA BADO ISHU
MKAZI mmoja kati ya watatu wa Manispaa ya Iringa anadaiwa kutokuwa na uelewa wa matumizi bora ya choo kwa kuwa hawana uhakika wa kuitumia huduma hiyo.

Watu hao kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela ni wale wanaoishi katika maeneo ya pembezoni mwa Manispaa hiyo inayozungukwa na wilaya za Iringa, Kilolo na Mufindi.

Alitoa taarifa hiyo juzi kwenye maadhimisho ya siku ya choo duniani, ambayo mjini Iringa yalifanyika katika viwanja vya shule ya Msingi Mtwivilla kwa uratibu wa wa asasi ya ACRA-CCS.

Asasi hiyo inayofadhiliwa na Jumuiya ya Ulaya (EU) inaendesha mradi wa miaka mitano wa usafi wa mazingira na usambazaji wa huduma ya maji mjini katika kata nne za majaribio za Nduli, Kihesa, Mtwivilla na Mkimbizi zilizoko pembezoni mwa Manispaa hiyo.

“Watu hao wanaishi kwenye hatari kubwa sana ikiwemo ya kupata magonjwa ya mlipuko, kwahiyo ni lazima takwimu hizo tuzifute kwa kuongeza jitihada zitakazowahakikishia watu hao huduma na matumizi ya vyoo bora,” alisema.

Kasesela alisema takwimu zinaonesha kuwa matumizi ya choo bora hupunguza magonjwa ya kuhara kwa asilimia 32 na kunawa mikono kwa sabani hupunguza magonjwa hayo kwa asilimia 50.

“Watu lazima wajue kwamba huduma na matumizi ya choo bora ni starehe. Ninapopata huduma hiyo nyumbani kwangu, huwa nafanya na mambo mengine kama kusoma magazeti na vitabu kwa kuwa nimeiboresha kwa kiwango kinachonipa starehe,” alisema.

Alizitaja sifa za choo bora kuwa ni kile kinachotunza faragha, chenye ubora, kisafi na kinachoongeza heshima kwa mmiliki wake.

Alimpa miezi sita mkurugenzi wa manispaa ya Iringa kuhakisha hamasa inafanywa kwa wasio na  huduma hiyo, wajenge vyoo na maeneo ya huduma kama mashule, yanakuwa na huduma bora za vyoo.

Awali Mtaalamu wa Masuala ya Habari wa ACRA-CCS, Joseph Makanza alisema katika kata hgizo mradi wao unalenga kutambua mifumo ya usafi wa mazingira, kuimarisha mnyororo wa utoaji wa huduma za usafi wa mazingira, kusaidia kubadili tabia katika jamii na kuongeza upatikanaji wa huduma za usafi wa mazingira na maji.

Makanza alisema huduma ya maji na usafi wa mazingira inahusisha matumizi ya teknolojia rahisi nay a bei nafuu kuujenga wa vyoo bora vitakavyomaliza tatizo la baadhi ya watu kujisaidia mahali popote pasipo na huduma hiyo.

Afisa Afya wa Manispaa ya Iringa, Ngilla Bwire alisema sehemu kubwa ya watu wanakidhi haja zao kwenye maeneo yasio rasmi ni wale wasio na makazi ya kudumu.

Meneja wa mradi huo, Joerg Henkel alinukuliwa siku za karibuni akisema mradi huo unatarajia kuwafikiwa watu 53,000 wanaounda kaya 11,00 ambao ni sawa na asilimia 32 ya wakazi wote wa manispaa ya Iringa na utalenga shule za msingi 48 zenye wanafunzi 40,000 na vituo vya afya na usafi 25.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment