Wednesday, 23 November 2016

MAONESHO YA UTALII WA KUSINI KUANZA NOVEMBA 25 MJINI IRINGA


WADAU mbalimbali wa sekta ya utalii wanazidi kujitokeza kushiriki maonesho ya utalii ya Nyanda za Juu Kusini (Karibu Kusini Tanzania Southern Circuit) yatakayofanyika kwa mara ya kwa mara ya kwanza mjini Iringa kati ya Novemba 25 na 29, mwaka huu. 

Mbali na hifadhi mbalimbali za Taifa, wadau wengine waliojitokeza na wanaoendelea kujitokeza ni wale wanaotokana na shughuli zinazohusiana na sekta hiyo wakiwemo watoa huduma.

Akizungumza na wanahabari jana, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alisema pamoja na changamoto ya rasilimali fedha, maandalizi ya maonesho hayo  yatakayofanyika katika viwanja vya Kichangani, mjini Iringa yanaendelea vizuri.

Masenza alisema Waziri wa Maliasili na Utalii Jumanne Maghembe anatarajia kuwa mgeni rasmi kwenye uzinduzi wa maonesho hayo yatakayokwenda sambamba na wiki ya utalii duniani.

Alisema mkoa wa Iringa kwa kushirikiana na mikoa mingine yote ya Nyanda za Juu Kusini, umeanzisha maonesho hayo yatakayokuwa yakifanyika kila mwaka ukiwa ni mkakati wao wa kuhamasisha utalii wa vivutio vya kusini mwa Tanzania.

Masenza alisema uamuzi huo umefanywa baada ya mkoa huo, mwaka 2009 kuteuliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kuwa kitovu cha utalii kwa mikoa ya Ruvuma, Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa inayounda kanda hiyo.

“Sisi wa mikoa ya Nyanda za juu kusini kwa kushikiana na Wizara ya Maliasili na utalii pamoja na wadau mbalimbali tunaandaa maonyesho…lengo la maonyesha hayo ni kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo mikoa ya Nyanda za juu kusini ili vijulikane kwa wageni na wananchi, ndani na nje ya Tanzania”  alisema.

Akifafanua kuhusu vivutio vilivyopo katika mikoa hiyo, Masenza alisema vipo vya kihistoria, kiutamaduni, na kiikolojia.

“Vivutio vya kihistoria na kiutamaduni vinahusisha vile vya mfumo mzima wa utawala na upiganiaji uhuru tangu enzi za vita vya chifu Mkwawa na vita vya maji maji dhidi ya wakoloni” alisema.

Kwa upande wa vivutio vya Ikolojia Masenza alisema mikoa hiyo inahifadhi ya taifa kubwa kuliko zote hapa nchini na Afrika Mashariki ya Ruaha ambayo pia ni ya pili kwa ukubwa barani Afrika.

Vingine ni pamoja na hifadhi ya Kitulo na Udzungwa; zana za mawe za kale pamoja na mapango, mcihoro na mito mikubwa.

Alisema vivutio hivyo vikitembelewa vitaongeza ajira kwa wananchi, mapato na kwamba vinatoa fursa za uwekezaji kama vitatumika ipasavyo kwa lengo la kuwezesha wananchi kujua umuhimu wa utunzaji wa maliasili na mazingira.

Aliwataka wadau wa ndani ya mkoa wa Iringa na nje kuungana na uongozi wa mikoa hiyo kwa ajili ya kufanikisha jukumu hilo alilodai ni muhimu kwa uchumi wa mikoa hiyo na taifa kwa ujumla.

Maandalizi ya sherehe za maadhimisho hayo yanafanywa kwa kupitia uratibu wa Kamati ya Utalii, Maliasili na Mazingira ya mkoa wa Iringa na Mradi wa Kuboresha Mtandao wa Maeneo ya Hifadhi Kusini mwa Tanzania (SPANEST).

Mratibu wa SPANEST, Godwel Ole Meing’ataki alisema “tunataka kuanza kwa mafanikio makubwa, na tunataka kuona wadau wa utalii wa mikoa hii wanashirikiana tofauti na ilivyosasa kwa kila mmoja kufanya mambo yake kivyake.”

Reactions:

0 comments:

Post a Comment