Tuesday, 29 November 2016

MAGHEMBE ATAKA BOMBERDIER ZITUE IRINGA KWA SH 300,000WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe ameomba ndege za serikali (Bomberdier) zianzishe safari ya kati ya Dar es Salaam na Iringa kwa Dola za Kimarekani 150 (sawa na zaidi ya Sh 300,000) ili kukuza utalii katika mikoa ya nyanda za juu kusini yenye vivutio lukuki.


Pamoja na ushauri huo amemkumbusha mmiliki wa hotel ya Peacock ya jijini Dar es Salaam, Joseph Mfugale kumalizia ujenzi wa hoteli ya nyota tano mjini Iringa ili kuboresha na kuongeza huduma za hotel ambayo ni moja ya changamoto zinazokwamisha ukuaji wa sekta hiyo mkoani Iringa.

Ujenzi wa hoteli hiyo inayojengwa karibu na Chuo Kikuu cha Katoliki cha Ruaha (RUCU) ulianza kwa kasi kubwa mwanzoni mwa mwaka 2008 lakini ukasimama miaka miwili baadaye.

Akizindua maonesho ya Karibu Kusini na Siku ya Utalii Duniani iliyoanza kufanyika kitaifa mjini Iringa juzi Novemba 27, Profesa Maghembe alisema huduma ya usafiri wa anga na ukosefu wa hoteli nzuri katika mikoa ya nyanda za juu kusini ni baadhi ya mambo yanayodhorotesha ukuaji wa sekta hiyo.

“Tunataka watalii toka nje waje kwa wingi kusini, lakini wanakwazwa na gharama kubwa za usafiri wa ndege, miundombinu mibovu ya barabara na huduma mbovu za hoteli,” alisema.

Profesa Maghembe aliahidi kulishauri shirika la ndege la taifa (ATC) kwa kupitia ndege zilizonunuliwa na zinazoendelea kununuliwa na serikali ya awamu ya tano kuanzisha safari za gharama nafuu Dar es Salaam, Iringa, Mbeya, Songwe, Njombe, Ruvuma na Katavi ili kuwahamasisha watalii kutembelea vivutio katika mikoa hiyo.

Hatua ya pili alisema ni kwa halmashauri za mikoa hiyo kutenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa hoteli zenye hadhi ya nyota nne na tano ili kuvutia watalii hasa wa nje huku akiwahakikishia wadau kwamba serikali na itaendelea kutengea fedha kwa ajili ya kukarabati miundombinu katika vivutio vya mikoa hiyo.

Kabla ya uzinduzi wa maonesho hayo, Profesa Maghembe alitembelea mabanda ya wadau mbalimbali yanayotangaza shughuli mbalimbali zinazohusiana na utalii nchini.

Awali Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza alisema mkoa wa Iringa kwa kushirikiana na mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, umeanzisha maonesho ya Karibu Kusini  yatakayokuwa yakifanyika kila mwaka ukiwa ni mkakati wao wa kuhamasisha utalii wa vivutio vya kusini mwa Tanzania.

Masenza alisema uamuzi huo umefanywa baada ya mkoa huo, mwaka 2009 kuteuliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kuwa kitovu cha utalii kwa mikoa ya Ruvuma, Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa inayounda kanda hiyo.

“Sisi wa mikoa ya Nyanda za juu kusini kwa kushikiana na Wizara ya Maliasili na utalii pamoja na wadau mbalimbali tunaandaa maonyesho…lengo la maonyesha hayo ni kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo mikoa ya Nyanda za juu kusini ili vijulikane kwa wageni na wananchi, ndani na nje ya Tanzania”  alisema.

Akifafanua kuhusu vivutio vilivyopo katika mikoa hiyo, Masenza alisema vipo vya kihistoria, kiutamaduni, na kiikolojia.

“Vivutio vya kihistoria na kiutamaduni vinahusisha vile vya mfumo mzima wa utawala na upiganiaji uhuru tangu enzi za vita vya chifu Mkwawa na vita vya maji maji dhidi ya wakoloni” alisema.

Kwa upande wa vivutio vya Ikolojia Masenza alisema mikoa hiyo inahifadhi ya taifa kubwa kuliko zote hapa nchini na Afrika Mashariki ya Ruaha ambayo pia ni ya pili kwa ukubwa barani Afrika.

Vingine ni pamoja na hifadhi ya Kitulo na Udzungwa; zana za mawe za kale pamoja na mapango, mchoro na mito mikubwa.

Alisema vivutio hivyo vikitembelewa vitaongeza ajira kwa wananchi, mapato na kwamba vinatoa fursa za uwekezaji kama vitatumika ipasavyo kwa lengo la kuwezesha wananchi kujua umuhimu wa utunzaji wa maliasili na mazingira.

Maadhimisho hayo yatakayofungwa kesho (leo Novemba 29) yanafanyika katika viwanja vya Kichangani mjini Iringa yakishirikisha wadau mbalimbali wa sekta ya utalii nchini.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment