Thursday, 24 November 2016

KITISI, KINYIKA KUKUTANA FAINALI YA SPANEST CUP

KITISI FC watakutana na Kinyika FC kwenye mchezo wa fainali ya kombe la SPANEST katika tarehe itakayotangazwa baadaye baada ya kumalizika kwa maadhimisho ya wiki ya Utalii, ambayo kitaifa yanafanyika mjini Iringa kati ya Novemba 27 na 29, mwaka huu.

Wakati Kitisi wamenusa fainali hiyo kwa mara ya pili baada ya kumchapa Mapagolo 5-1 katika mchezo uliopigwa Novemba 22, Kinyika imezima ndoto ya mabingwa wa mwaka 2014, Itundundu FC baada ya kuwachapa kwa mikwaju ya penati 4-3. Katika mchezo uliochezwa Novemba 23.

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela alitoa zawadi ya Sh 20,000 kwa mchezaji wa Itunundu, Said Kisogenze aliyekuwa wa kwanza kuona lango la wapinzani wao, Kinyika.

Mbali na mashindano hayo yaliyoshirikisha timu 24 zinazoundwa na vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, wilayani Iringa kuwasaidia wachezaji wake kujenga afya, yanatumika kusambaza unaolenga kuwaokoa Tembo dhidi ya majangili nchini kote.

Mratibu wa Mradi wa Kuboresha Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania (SPANEST) inayoratibu mashindano hayo, Godwell Ole Meing’ataki alisema fainali ya ligi hiyo inalenga kuoa Tembo kwa kupitia kauli mbiu yake ya “Piga Vita Ujangili, Piga Mpira Okoa Tembo.”

Meing’ataki alisema zawadi kwa mshindi wa kwanza atakayepata kombe, medali, seti moja ya jezi, cheti na kutembelea hifadhi ya Ruaha ataondoka na Sh Milioni moja taslimu, huku mshindi wa pili atakayepata medali, cheti na mipira miwili atakinyakulia Sh 700,000.

Alisema timu ya Mapogolo FC na Itunundu FC zitamenyana kusaka nafasi ya tatu ambayo mshindi wake atajipatia cheti na medali na Sh 500,000 taslimu huku.

Meing’ataki alisema wazo la kuunganisha vijana katika vita ya ujangili linaonekana kuwa njia muafaka ya kutokomeza ujangili kutokana na ukweli kwamba vijana ndiyo walengwa wakubwa katika kushawishika kuingia kwenye maeneo yaliyohifadhiwa na kufanya ujangili.


Alisema michezo hiyo itapigwa katika uwanja wa Kimande, Pawaga kwasababu ya kuowa na mashabiki wenye mwamko mkubwa wa mchezo huo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment