Saturday, 26 November 2016

KIKWETE AZUNGUMZIA TATIZO LA AJIRA ZA WALIMU

RAIS wa Awamu ya Nne na Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam, Dk Jakaya Kikwete amewapoza wahitimu wa fani ya ualimu akisema wasikatishwe tamaa na tatizo la ajira katika sekta hiyo kwa kuwa ni suala la muda litakalokwisha muda mfupi ujao.

Dk Kikwete aliyasema hayo leo alipokuwa akiwajibu wahitimu wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa waliopaza sauti wakimtaka amuombe Rais Dk John Magufuli afungue milango ya ajira katika sekta hiyo na sekta nyingine za umma.

Mmoja wa wahitumu hao (jina lake halikupatikana) alisema “inaumiza kuona wenzao waliomaliza chuo hicho mwaka mmoja uliopita wakiendelea kusoka mitaani na sasa tunaungana nao katika msoto huo.”

“Ujumbe umefika” Dk Kikwete aliyekuwa mgeni rasmi katika mahafali ya nane ya chuo hicho yaliyofanyika jana katika viwanja vya chuo hicho mjini Iringa. alisema.

Aliwaambia wahitimu 952 aliowatunuku vyeti vyao katika fani nne za shahada za elimu kwamba tatizo la uchelewaji wa ajira kwao litakwisha baada ya muda mfupi kwa kuzingatia kwamba Taifa lina mahitaji makubwa ya walimu.

Kikwete aliyetumia dakika sizisozidi tatu kuzungumza na wahitimu hao wakati akifunga mahafali hayo, alisema ataufikisha ujumbe huo kunakohusika kama alivyoombwa.

Akizungumzia maendeleo ya chuo hicho Mkuu wa chuo hicho, Profesa Bernadeta Killian alisema uongozi wa chuo unaendelea na mikakati mbalimbali ya kukiboresha ili kiendelee kuwa taasisi na mahali bora pa kutolea elimu, huduma za jamii kama vile ushauri na kuongeza udahili wa wanafunzi.

Alisema tangu kuanzishwa kwake mwaka 2006, chuo kimezalisha wahitimu 5018 kama walimu katika fani mbalimbali.

“Aidha idadi ya wanataaluma wenye shahada za uzamivu imeongezeka kutoka 0 mwaka 2006 hadi 26 mwaka huu,” alisema.

Pamoja na mafanikio hayo na mengine mengi, Profesa Killian alisema chuo kinaendelea kuikumbusha serikali kuwa ruzuku inayotolewa kwa ajili ya uendeshaji na utekelezaji wa mipango mbalimbali bado ni ndogo na imekuwa ikishuka mwaka hadi mwaka.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Usimamizi ya MUCE na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Profesa Rwekaza Mukandala  alisema MUCE wana changamoto ya uhaba wa walimu kiasi cha chuo kutumia wahadhiri kutoka vyuo vingine kwa gharama ya ziada.

Pia upungufu wa wafanyakazi waendeshaji na upungufu mkubwa wa ofisi za wanataaluma hali inayopelekea mazingira ya utendaji wa kazi kwao kuwa mgumu. 


Katika kukabiliana na changamoto hizo, Profesa Mukandala alisema chuo kimechukua hatia kadhaa zilizo ndani ya uwezo wake lakini ili kuzimaliza inahitaji msukomo kutoka serikalini.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment