Tuesday, 29 November 2016

CHIKU ABWAO AONDOLEWA CLUB VIP, AKIMBILIA MAHAKAMANI

Tokeo la picha la Chiku AbwaoALIYEKUWA mbunge wa viti maalumu kwa nyakati tofauti mkoani Iringa kwa kupitia chama cha NCCR-Mageuzi na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chiku Abwao amevunjiwa mkataba wa upangaji katika jengo la Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mjini Iringa baada ya kutuhumiwa kukiuka masharti ya upangaji.

Abwao alikuwa mpangaji wa jengo lenye Club maarufu ya VIP lililopo Plot Na 36 katika mtaa wa Haile Sellasie, kata ya Gangilonga, mjini Iringa; na kinyume na masharti ya mkataba akapangisha jengo hilo kwa mtu mwingine aliyetajwa kwa jina la Alex Mgeta na kujipatia mamilioni ya shilingi.

Juzi asubuhi, Abwao alijaribu kudhibiti mkataba wake kwa kufunga makufuli yake juu ya makufuli ya Club hiyo, hatua iliyosababisha uongozi wa Club hiyo kutoa taarifa hiyo Polisi na NHC kabla ya kuchukua hatua za kuvunja makufuli hayo.

Pamoja na kufunga jengo hilo, Abwao aliweka ulinzi kwa kutumia kampuni binafsi ya ulinzi ili wahusika wasivunje makufuli hayo na kuingia ndani akidai kwamba biashara ni yake na katika jengo hilo kuna mali zake nyingi yakiwemo makreti ya bia na soda, viti na meza.

Ukiwa na uongozi wa NHC, majira ya saa nane mchana , uongozi wa club hiyo ulifanikiwa kuvunja makufuli hayo, ukaifungua club hiyo na kuendelea na shughuli zake kama kawaida.

Kaimu Meneja wa NHC Mkoa wa Iringa, Lepson Usia alisema shirika lao liliamua kuvunja mkataba na Abwao baada ya kubaini amevunja baadhi ya masharti ya upangaji.

“Mama Chiku alikuwa mpangaji wetu na kwa makasudi aliamua kumpangisha mtu mwingine ili aweze kupata manufaa. Baada ya kulitambua hilo tumeamua kuvunja mkataba na kumpangisha mpangaji aliyempangisha,” alisema.

Usia alisema ni kosa kwa mujibu wa taratibu za shirika hilo kumpangisha mtu mwingine na akatoa wito kwa wapangaji wao kutofanya kosa hilo kwani wakibainika watachukuliwa hatua kama iliyochukuliwa kwa Abwao.

Awali Msimamizi wa Club VIP , Leonard Lukasola alisema waliingia mkataba wa siri wa upangaji wa jengo hilo na Chiku Abwao kwa muda wa miaka mitatu.

“Tukiwa katika mkataba huo wa siri, NHC walifanya ukaguzi kwa kuangalia nyaraka mbalimbali  ikiwemo leseni na kubaini anayefanya biashara katika jengo hilo sio Chiku Abwao,” alisema.

Alisema baada ya kubaini hilo, NHC walitoa notisi ya kumuondoa katika jengo hilo Abwao; Notisi iliyoisha Novemba 24, mwaka huu na kwa mujibu wa taratibu wametoa mkataba kwa mpangaji waliyemkuta.

“Kwa kupitia mkataba na Chiku Abwao, mwaka wa kwanza tulilipa Sh Milioni 19, mwaka wa pili tulilipa Sh Milioni 24 na mwaka wa tatu ulioisha hivikatibuni tulilipa Sh Milioni 27, wakati yeye alilipa kati ya Sh Milioni 8 na Sh 14 kwa mwaka kwa kipindi hicho kwa mujibu wa taarifa zilizopo NHC” alisema.

Alipotafutwa  kuzungumzia sakata hilo, Abwao alisema hajawahi kuwa na mkataba wa ubia wa kibiashara na mpangaji aliyepewa mkataba mpya na NHC bali alikuwa akifanya naye kazi kama promota wa biashara zake katika jengo hilo linalotumiwa pia na wasanii wa muziki kutoa burudani.

Kuhusu kujipatia mamilioni ya shilingi baada ya kumpangisha mpangaji mwingine, Abwao alisema fedha alizokuwa akilipwa na Promota huyo hazikuwa za kodi pakee yake kwani zilihusisha na mapato yatokanayo na na faida yao ya kibiashara.


“Nimeweka pingamizi mahakamani kupinga uamuzi wa NHC wa kunitoa kinyemela na nimeripoti suala hili Takukuru kwasababu nahisi kuna harufu ya rushwa,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment