Thursday, 17 November 2016

BAADA YA FIESTA YA CLOUDS FM, TIGO YADHAMINI MTIKISIKO WA EBONY FM


BAADA ya kudhamini tamasha la kila mwaka la FIESTA, Kampuni ya Tigo Tanzania imetangaza udhamini wa tamasha la Mtikisiko linalolenga kuinua wanamuziki chipukizi wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.

Tamasha hilo litakalofanyika katika kipindi cha mwezi mmoja katika mikoa ya Ruvuma, Njombe, Iringa na Mbeya linaratibiwa na Redio Ebony FM ya mjini Iringa.

Akizungumza na wanahabari jana, Mkurugenzi wa Tigo wa Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, Jackson Kiswaga alisema udhamini wa tamasha hilo litakaloanzia Makambako mkoani Njombe, Jumamosi ni sehemu ya sera ya kampuni hiyo ya kusaidia makundi mbalimbali ya jamii wakiwemo vijana na wasanii ili wafikie ndoto zao za maisha.

Kiswaga alisema Tigo italitumia tamasha hilo kama nyenzo ya kuwasaidia wanamuziki wapya kutoka katika mikoa hiyo kwa kuwatambulisha mbele ya mashabiki na hivyo kuwaweka katika nafasi ya kujipatia kipato kutokana na kazi zao.

“Udhamini huu umeonesha ni jinsi gani Tigo imedhamiria kusaidia kuendeleza mikakati na shughuli mbalimbli za ubunifu zinazofanywa na vijana katika harakati zao za kujiinua kiuchumi katika kipindi ambacho Rais Dk John Magufuli ameahidi kusaidia na kulinda kazi za wasanii,” alisema.

Alisema mapema mwaka huu, kampuni ya Tigo ilizindua huduma iitwayo Tigo Music ambayo inawapa wanamuziki fursa ya kupakia nyimbo zao kwenye mtandao wao wa Internet na hivyo kuweza kusikilizwa na hadhira ya kitaifa na kimataifa jambo linalowapa wasanii kipato cha ziada na fursa ya kujulikana kimataiafa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Tamasha hilo, Bonny Zakaria alisema Ebony FM inatumia matamasha hayo ya Mtikisiko kurudisha fadhira kwa wasikilizaji na wateja wao.

“Tulianza na mkoa wa Iringa na kwa kadri matangazo yetu yanavyotanuka, Mtikisiko tunaufanya pia katika mikoa ya Mbeya, Njombe na Songea huku lengo letu ni kufika katika mikoa yote nchini,” alisema.

Alisema mbali na kuwatangaza wanamuziki chipukizi, tamasha hilo litakalohusisha wasanii mbalimbali wakubwa akiwemo Mr Blue, Chege, Darasa na wengineo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment