Tuesday, 18 October 2016

WANAOUZA GESI YA KUPIKIA BILA KUWA NA MIZANI KULIMWA FAINI YA SH MILIONI 5


MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) itaanza kutoa bei kikomo kwa gesi za kupikia zinazotokana na zao la mafuta ya Petroli, utaratibu unaotarajia kuanza Januari mwakani.

Ikitangaza utaratibu huo, mamlaka hiyo imesema muda wote, katika miundombinu ya kujazia gesi ya kupigia na vituo vya kuuzia gesi ni lazima pawepo mizani inayoweza kupima uzito wa mitungi ya gesi.

Mkurugenzi wa Idara ya Petroli wa Ewura, Godwin Samweli alisema mjini Iringa wakati mamlaka hiyo ilipofanya semeni na wafanyabiashara wa mafuta wa mikoa ya Iringa na Njombe kwamba mizani hiyo ni lazima iwe imehakikiwa na kuwekwa lakiri ya Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA).

Alisema kutokuwa na mizani hiyo ni kosa kisheria na adhabu kwa kosa la kwanza ni faini isiyopungua Sh Milioni 3, kosa la pili faini isiyopungua Sh Milioni 5 na mkosefu mzoefu atanyang’anywa leseni.

Akifafanua kuhusu udhibiti wa bei ya gesi ya kupikia, Samweli alisema baada ya EWURA kufanya mkutano na wadau wa sekta hiyo baadaye mwaka huu, itakamilisha kanuni ya kupanga bei zitakazoanza kutumika mapema mwakani.

Alisema mpango huo unakuja baada ya EWURA kutengeneza utaratibu utakaoifanya Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) kuanza kuanza kuingiza gesi ya kupikia kwa wingi.

“Bei hizo zitakuwa zikitangazwa kama zile za mafuta ya Petroli lakini kwasasa wafanyabiashara wazingatie bei zinazotolewa na kampuni zinazowauzia gesi,” alisema.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment