Tuesday, 18 October 2016

WAMILIKI WA SHULE, VYUO NYANDA ZA JUU WAANZISHA SACCOS


WAMILIKI wa shule na vyuo binafsi vilivyoko Nyanda ya Juu Kusini (TAMONGSCO) wameanzisha Chama cha Akiba na Mikopo (Saccos) wakilenga kiwasaidie kuboresha shughuli zao na kukabiliana na urasimu wa taasisi zingine za kifedha hasa mabenki.

Katika mkutano wao wa kupitisha katiba ya Saccos hiyo uliofanyika mjini Iringa hivikaribuni, wamiliki hao walisema riba kubwa na masharti lukuki wanayopewa na mabenki ili wapate mikopo yanakwamisha mipango ya kuboresha huduma zao.

Mwenyekiti wa TAMONGSCO, Lucas Mwakabungu alisema “tumeamua kuanzisha chombo chetu cha kifedha kitusaidie pale tunapokosa huduma za kibenki kwa wakati, ni matarajio yetu kitakuwa mkombozi mkubwa kwa wale wote wanaoshindwa masharti ya mabenki.”

Alisema katika kipindi cha miezi sita ijayo, wanatarajia kukusanya zaidi ya Sh Milioni 500 kutoka kwa wanachama wake zaidi ya 20.

Mwakabungu alisema kiasi hicho cha fedha kitaiwezesha Saccos hiyo kusimama na kuanza kutekeleza wajibu wake kwa wanachama wake kwa kuzingatia taratibu na kanuni watakazojiwekea.

Alisema hakuna shaka kwamba Saccos hiyo itakuwa mkombozi mkubwa kwa wamiliki hao ambao wengi wao wamekuwa wakiyaona mabenki kama vikwazo vya maendeleo yao kutokana na riba na muda mrefu wa upataji wa mikopo.

“Tunataka kilio chetu kimalizike kupitia Saccos hii, kwahiyo ni wajibu wetu kuhakikisha tunasimamia misingi ya uanzishaji wa chombo hiki ili kiwe cha manufaa sasa na miaka mingi ijayo,” alisema.

Alisema wanachama wa Saccos hiyo kwa umoja wao ni wamiliki wa taasisi hiyo itakayowaondoa na adha na karaha za taasisi kubwa za kifedha.
  
 Naye katibu wa TAMONGSCO wa kanda hiyo, Nguvu Chengula ambaye ni mmiliki wa shule ya Sun Academy alisema shule nyingi hukumbwa na uhaba wa fedha mwishoni mwa mwaka hali inayozorotesha uendeshaji wake.

Kutokana na changamoto hiyo, Chengula alisema wamiliki wengi hujikuta wakilazimika kukopa fedha za mitaani kwasababu ya kushindwa kumudu masharti ya kibenki.

Kwa upande wake Noah Mtokoma ambaye ni mwenyekiti wa saccos hiyo alisema kuwa uaminifu na uadilifu ndicho kitu cha muhimu kitakachoifanya Saccos hiyo ikue na iwe kimbilio la wanachama wake.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment