Thursday, 20 October 2016

WAHISANI WAZUNGUMZIA SAKATA LA LEMA NA GAMBO ARUSHA


WAHISANI wakuu katika mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Mama na Mtoto, Jijini Arusha wameibuka na kudai kuwa kulikuwa na upotoshwaji mkubwa kuhusiana na mchakato wa mradi huo.

Haya yanakuja siku moja baada ya kuibuka kwa mzozo kati ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo katika zoezi la uwekaji msingi wa mradi huo mbele ya wahisani hao. Mwenyekiti wa Bodi ya Maternity Africa, Profesa Wilfred Mlay amesema wanatarajia kuwa na kikao wiki ijayo na kutoa taarifa rasmi kwa vyombo vya habari juu ya mradi huu na ushiriki wa taasisi mbalimbali kwa lengo la kuweka kumbukumbu sawa.

 “Tumejifunza, sasa tutawasiliana na viongozi wa juu wa Serikali ikiwamo Wizara husika ili kuona mradi huu hauvurugwi ama kuingiliwa hadi kukamilika kwake,” amesema.

Pamoja na hilo, Mlay amedai kuwa mchango wa ArDF katika mradi huo unajulikana na kwamba ndiyo taasisi iliyoshiriki katika hatua zote ikiwemo kubadili hati za kiwanja hicho kuwa cha Maternity Africa.

 “Kitu ambacho kilijitokeza ni upungufu wa hekima, ilitakiwa kuangalia lengo la jambo badala ya kutumia tukio hilo kama ngazi ya kisiasa na kuibua jambo ambalo halipo,” amesema Mlay na kuongeza kuwa katika mradi huo hakuna mchango wa Global Fund wala taasisi ya Bill Gate na Mkewe Melinda kama ilivyokuwa imeainishwa.

Juzi akizindua ujenzi wa mradi huo utakaogharimu zaidi ya bilioni 9, Gambo alisema ardhi kwa ajili ya Hospitali hiyo ilitolewa na taasisi hiyo Mawalla Fund na kwamaba suala la afya ya mama na mtoto lilikuwa maono ya muda mrefu ya Wakili huyo na kudai kuwa watu wa Mawalla wanapongezwa na wanatambulika kama watu muhimu kwakuwa wangeweza kutoa ardhi hiyo kwa shughuli nyingine.

Aliongeza kuwa taasisi ya Mawalla ndiyo iliyoanza mazungumzo na wadau kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo na kwamba ingesaidiwa na bilionea wa Marekani, Bill Gates na Mkewe Melinda na kusisitiza kuwa ni vyema taasisi ya Maternity Africa wakaendesha ujenzi huo bila kuingiza siasa.

Kutokana na kauli hiyo ndipo viongozi wa Mfuko wa Maendeleo Arusha (ArDF) Lema na Mwenyekiti Elifuraha Mlowe walikerwa na kudaikuwa Mkuu wa Mkoa huyo alikuwa anapotosha ukweli wa jambo hilo kwa misingi ya kisiasa na kwamba taasisi yao ndiyo iliyotoa ardhi hiyo baada ya kukabidhiwa na Mawalla.


“Mimi ndiye niliyetafuta ardhi na nilikabidhiwa ardhi na nyote mtakumbuka nilipokuja kukabidhiwa hapa,” alisema Lema akipinga vikali kauli ya Gambo mbele ya wahisani hao.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment