Friday, 28 October 2016

UGOMVI WA MIPAKA KILOLO WAFIKIA ASILIMIA 61ASILIMIA 61 ya migogoro yote ya ardhi wilayani Kilolo mkoani Iringa, imeelezwa na mtandao wa Mashirika yasiyokuwa ya Kiserikali yanayofanya kazi na wakulima na wafugaji wadogo nchini Tanzania (PELUM Tanzania) kwamba inatokana na ugomvi wa mipaka katika maeneo ya vijijini.

Akiwasilisha mada katika mdahalo uliofanywa wilayani humo ukilenga kutafuta mambo yakufanya ili kupunguza malalamiko ya migogoro ya ardhi, Afisa Mradi wa PELUM Tanzania, Angolile Rayson alisema:

“Katika kuhakikisha wananchi wanakabiliana na changamoto hiyo shirika lake limetoa elimu, na kuimarisha kamati za ardhi za vijiji na mabaraza ya ardhi ya vijiji ili yaweze kutatua migogoro pindi inapojitokeza kwenye maeneo yao.

Rayson alisema mafunzo hayo ya haki za ardhi na utawala yanalenga kuwaongezea wananchi wa wilaya hiyo uelewa juu ya sheria za ardhi, haki za ardhi kwa wanawake na makundi maalum pamoja na utatuzi wa migogoro ya ardhi.

Kwa ufadhili wa shirika la Kimataifa la Maendeleo la Marekani (USAID), alisema wilayani humo; mtandao huo umekuwa ikitoa mafunzo hayo katika vijiji vya Ikuka, Mbigili, Mawala, Mawambala na Masalali kwa kupitia mradi wake wa CEGO unaohusisha jamii ya vijijini katika uwajibikaji wa masuala ya ardhi ya kijiji.

Wakichangia mada, wakazi wa wilaya hiyo wamesema migogoro ya ardhi katika maeneo yao itakoma kama serikali itasimamia kwa nguvu zake zote utekelezaji wa sheria za ardhi hatua ambayo pia itaimarisha amani na utulivu na kuifanya sekta hiyo kuwa na tija kwa jamii.

Kwa upande wake, Charles Mkoga alizituhumu serikali za vijiji akisema ni chanzo cha migogoro kwasababu zina baadhi ya viongozi wanaoshindwa kusimamia sheria hizo baada ya maamuzi kufanywa.

“Wakati mwingine serikali hizi zimekuwa zikitoa maamuzi ya matumizi ya ardhi bila kuzingatia sheria na kwa kweli zipo ambazo hazishirikishi kabisa wananchi wake katika maeneo husika,” alisema.

Kwa upande wake Bahati Mkove aliomba serikali kwa kutumia sheria hizo hizo kutenga maeneo kwa ajili ya wakulima na wafugaji  hatua itakayosaidia makundi hayo kuepukana na migogoro kwa kuwa makundi yote mawili yanategemeana.

Meneja miradi wa PELUM Tanzania iliyoandaa mdahalo huo, Rehema Fedelisi alisema shirika lake limeamua kufanya kazi hiyo kwa lengo la kusaidia kukuza uelewa wa wananchi juu ya ya haki zao kwa masuala yahusuyo ardhi na mbinu za kukabiliana nayo ili kupunguza tatizo hilo nchini.

Alisema kwa sasa mradi huo unatekelezwa katiak vijiji 30 vilivyopo katika wilaya sita za mikoa mitatu ya Tanzania bara na kwamba tangu utekelezaji huo umeanza mwaka 2013 watu wengi wameelimika na kuanza kutambua haki zao na kutatua migogoro inayohusu maeneo yao.

Akifungua mdahalo huo Katibu Tawala wa Wilaya ya Kilolo, Yusuph Msawanga aliwataka washiriki wa madahalo huo kutumia fursa hiyo kutoa changamoto zilizopo katika sekta ya ardhi kama njia ya kuzitafutia ufumbuzi.


“Migogoro mingi ya ardhi imekuwa ikitokea kuanzia ngazi ya familia, jamii, kijiji kwa kijiji na hata wilaya kwa wilaya…shirika hili licha ya kutupatia elimu bado leo limetukusanya ili tutoe mawazo yetu yatakayosaidia kumaliza migogoro hiyo”alisema Msawanga.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment