Friday, 21 October 2016

RATIBA YA AWAMU YA PILI YA KOMBE LA KUPIGA VITA UJANGILI YATANGAZWA





MRADI wa Kuboresha Maeneo Yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania (SPANEST) umetangaza rasmi ratiba ya ligi ya kombe la SPANEST kwa msimu wa 2016, itakayokuwa na jumla ya timu 24 badala ya 21 za msimu uliopita.

Ligi hiyo inayolenga kuoa Tembo kwa kupitia kauli mbiuz yake ya “Piga Vita Ujangili, Piga Mpira Okoa Tembo” imepangwa kuanza Oktoba 23 mwaka huu na itachezwa kwa mwezi mmoja kwa uratibu wao na usimamizi wa Chama cha Mpira wa Miguu Iringa Vijijini (IRFA).

Mratibu wa SPANEST, Godwell Ole Meing’ataki alisema mradi umeongeza mara dufu zawadi ya fedha taslimu kwa mshindi wa kwanza hadi wa tatu wa ligi hiyo inayoshirikisha timu hizo zinazoundwa na vijiji vinavyozunguka hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Meing’ataki alisema zawadi kwa mshindi wa kwanza atakayepata kombe, medali, seti moja ya jezi, cheti na kutembelea hifadhi ya Ruaha imeongezeka kutoka Sh 300,000 hadi Sh Milioni moja.

Kwa upande wa mshindi wa pili atakayepata medali, cheti na mipira miwili imeongezeka kutoka Sh 200,000 hadi Sh 700,000 na ya mshindi wa tatu anayepata cheti na medali imeongezeka kutoka Sh 100,000 hadi Sh 500,000.

Naye Kaimu Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Moronda Moronda alisema wazo la kuunganisha vijana katika vita ya ujangili linaonekana kuwa njia muafaka ya kutokomeza ujangili kutokana na ukweli kwamba vijana ndiyo walengwa wakubwa katika kushawishika kuingia kwenye maeneo yaliyohifadhiwa na kufanya ujangili.

Akipokea kombe na vifaa vingine kwa ajili ya ligi hiyo inayowaunganisha vijana katika vita dhidi ya ujangili wa wanyamapori, Katibu wa IRFA, Juma Lalika alisema uzinduzi wa ligi hiyo utazikutanisha timu za kijiji cha Kimande na Itunundu ambaye ni bingwa mtetezi, mchezo utakapigwa katika kijiji cha Kimande.

Katibu tarafa wa Idodi, Yacob Kiwanga na wa tarafa ya Pawaga, Alli Ngweja ambao tarafa zao zinaunda vijiji hivyo vinavyoshiriki ligi hiyo, walishiriki shughuli ya makabidhiano ya vifaa hivyo iliyofanyika katika ofisi ya SAPNEST, mjini Iringa juzi.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment