Thursday, 13 October 2016

MUFINDI WAFURAHIA HUDUMA ZA CRDB BENKI

BAADHI ya wananchi wanaoishi katika vijiji vya wilaya ya Mufindi mkoani Iringa wameipongeza benki ya CRDB kwa namna inavyosogeza huduma za kibenki jirani na makazi yao hatua waliyoeleza inawaongezea usalama wa fedha zao.

Wilaya ya Mufindi ni moja kati ya wilaya viwanda vikubwa na vidogo inayoelezwa kuwa na mapato makubwa yanayotokana na biashara za mazao ya misitu, chai, kahawa, pareto na mazao ya chakula kama mahindi na mazao ya mbogamboga.

Meneja wa CRDB tawi la Mafinga, Cosmas Ngimba alisema “CRDB benki ilifungua tawi lake la kwanza mjini Mafinga miaka miwili iliyopita ili kurahisisha huduma kwa wananchi wa wilaya hiyo.”

Ngimba alisema ili kuwafikia wananchi wa mbali na Mafinga mjini, benki hiyo  imefungua tawi dogo katika kijiji cha Lugoda na ina mawakala wanaotoa huduma za kibenki katika vijiji mbalimbali kikiwemo kijiji cha Sawala, Kilimani, Igowole na Ludilo huku wakiendelea na taratibu za kuwa na mawakala katika kila kijiji.

“Waliokuwa wanafuata huduma Mafinga Mjini wakiwa na fedha kwenye mabegi na mifuko yao, sasa wanapata huduma jirani kabisa na maeneo wanayoishi,” alisema.

Wakizungumza na gazeti hili baada ya maadhimisho ya wiki ya huduma kwa mteja yaliyofanyika hivikaribuni, wananchi hao wamesema kabla ya utaratibu huo wengi wao walikuwa na kawaida ya kuhifadhi fedha zao ndani ya vyumba vyao.

“Ilikuwa ni hatari kukaa na fedha majumbani au kusafiri na fedha umbali merufu kwa ajili ya kupata huduma za kibenki,” alisema Maulid Juma mmoja wa wafanyabiashara wa wilaya hiyo.

Naye Nickson Witara mkazi wa kijiji cha Igowole alisema mawakala wa benki hiyo wamekuwa wakombozi kwa wakazi wa vijijini kwani wanaweza kuweka na kutoa fedha zao kwa kutumia pia mitandao ya simu.

“Hatuna sababu tena ya kusafiri hadi Mafinga mjini kufuata huduma za kifedha, ombi letu kwa CRDB ifungue matawi na iongoze mawakala katika maeneo mengi vijijini,” alisema.

Afisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, Lucy Timba alisema mbali na ufunguzi wa matawi na utaratibu wa mawakala kurahisisha huduma ya kifedha kwa watumishi ambao ni wateja wa benki hiyo, benki hiyo imesaidia kupunguza malalamiko kwa watu wengi waliokuwa wanasafiri umbali mrefu kufuata huduma.

“Ushauri wangu kwa vijana wajasiriamali wa wilaya hii, watumie benki kuhifadhi fedha zao kwani mbali na kujihakikishia usalama wa fedha hizo, wanajiweka katika mazingira ya kuaminika na kukopesheka,” alisema.


Katika maadhimisho ya wiki hiyo, CRDB tawi la Mafinga imewafariji wafungwa na wagonjwa kwa kutoa misaada mbalimbali ikiwemo mafuta ya kupaka, miswaki dawa za meno, sabuni na sukari.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment