Wednesday, 12 October 2016

KOPE BANDIA HATARI KWA USALAMA WA MACHO

image

WAKATI watanzania wakiungana na dunia kuadhimisha siku ya afya ya macho duniani kesho alhamisi, wanawake wametakiwa kujiepusha na matumizi ya kope bandia kwasababu ni hatari kwa usalama wa macho yao.

Siku ya afya ya macho duniani ni siku ya kimataifa inayofanyika kila alhamisi ya pili ya mwezi Oktoba ya kila mwaka kwa lengo la kuhamasisha jamii kujihadhari na magonjwa ya macho.

Akizungumza na wanahabari kuhusu maadhimisho hayo yatakayofanyika kimkoa kesho (leo alhamis) katika hospitali ya mkoa wa Iringa, Mratibu wa Huduma za Macho wa Mkoa wa Iringa Dk George Kabona alisema matumizi ya kope bandia yanaweza kusababisha upofu.

Alisema kope bandia hupandikwa juu ya kope halisi za mwanamke kwa kutumia gundi maalumu inayoweza kusababisha madhara ndani au nje ya jicho yanayoweza kuleta magonjwa ya macho ikiwa ni pamoja na kupoteza uwezo wa kuona.

Dk Kabona alisema wakati mkoa wa Iringa una zaidi ya wasioona 9000, takwimu za kitaifa zinaonesha wanne kati ya watano wana upofu unaoepukika.

“Tunahitaji kuwekeza kwenye huduma za afya ya macho kwa kuongeza bajeti zetu kwenye mfumo wa huduma wa umma,” alisema.

Akitoa mfano, Dk Kabona alisema wakati hospitali ya mkoa wa Iringa inahitaji zaidi ya Sh Milioni 20 kwa mwaka kwa ajili ya kutoa huduma za macho, imekuwa ikipata wastani wa Sh Milioni 2 kwa mwaka.

Katika kuadhimisha siku ya macho, alisema wanawahamasisha wagonjwa wa kisukari kufika katika hospitali hiyo na kufanyiwa uchunguzi na kuanzishiwa mchakato wa matibabu kwa kuwa ugonjwa huo ni moja ya magonjwa yanayosababisha upofu.


Aliyataja magonjwa mengine yanayosababisha upofu kuwa ni pamoja na mtoto wa jicho, makovu kwenye kio cha jicho, presha ya jicho, upeo mdogo wa kuona, kisonono cha macho, saratani ya jicho na magonjwa mengineyo yanayosababishwa na umri mkubwa.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment